Stars kwa Namibia kitaeleweka tu!

WAKATI kocha wa timu ya taifa ya Namibia, Richard Bobby Samaria akiitolea macho Tanzania watakayovaana nayo leo kwenye mfululizo wa mechi za Fainali za Chan, Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije amesisitiza mechi hiyo lazima kieleweke ili wasing’olewe.

Timu hizo zitavaana kwenye mechi ya Kundi D, huku zote zikiwa zimetoka kupoteza mechi zao za awali, Namibia ikifungwa mabao 3-0 na Guinea huku Stars ikicharazwa 2-0 na Zambia na yeyote anayepoteza mchezo wa leo ataungana na Zimbabwe kuziaga fainali hizo.

Matokeo hayo ya kichapo katika mchezo wa kwanza, yaliitupa Namibia mkiani mwa msimamo wa kundi D nyuma ya vinara Guinea, Zambia iliyopo nafasi ya pili na Stars ikiwa ya tatu na kesho timu hizo zitakwaruzana kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Wakizungumza kuelekea mchezo huo, makocha wa timu hizo wametambiana, huku Ndayiragije akiwatoa hofu Watanzania kwa kuwaambia kwamba wamejipanga vyema ili kuona wanatoka na ushindi kuweka hai matumaini yao ya kuendelea kuwepo michuanoni.

Kocha huyo alisema ameridhishwa na kiwango cha timu yake licha ya kupoteza dhidi ya Zambia na watahakikisha wanaibuka na ushindi katika mechi mbili zinazofuata wakianza na Namibia kisha kumalizana na Guinea Jumatano ijayo.

“Mechi yetu na Zambia ilikuwa ni 50/50 na wapinzani wetu waliweza kutumia vyema nafasi walizopata. Timu zote mbili zilicheza mpira mzuri na mashabiki walifurahia walichokiona.

“Tunatakiwa kufanya kazi ya ziada kwa sababu tuna mechi mbili za kucheza kwenye kundi na tuna nafasi,” alisema Ndayiragije ambaye ni raia kutoka Burundi.

Kwa upande wa Namibia, Kocha Samaria alisema wanaupa uzito mkubwa mchezo dhidi ya Tanzania kwani ndio umeshikilia hatima yao kwenye mashindani hayo.

“Tumejifunza kutokana na matokeo yetu dhidi ya Guinea. Tumefungwa mabao mawili kutokana na makosa ya kizembe. Hakuna cha kulaumu katika hili lakini tumepoteza dhidi ya timu ya Guinea iliyoandaliwa vizuri.

Tunatakiwa kurudi kujipanga na mchezo wetu unaofuata dhidi ya Tanzania ambao nao wamepoteza mechi iliyopita,” alisema Samaria.

Timu hizo za Tanzania na Namibia zinashiriki fainali hizo za Chan kwa mara ya pili, Stars ikishiriki mara ya kwanza 2009 na Namibia katika fainali zilizopita na kukwamia robo fainali.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 ilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo, ambapo ilitolewa katika hatua ya makundi.