Singida yatakata nyumbani, Bruno amlilia Pele

KIUNGO mshambuliaji wa Singida Big Stars, Bruno Gomes raia wa Brazil ameendelea kuwa moto wa kuotea mbali baada ya kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Geita Gold

Singida BS imeibuka na ushindi huo leo katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, ukiwa ni ushindi wa pili mfululizo baada ya Jumatatu kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Gomes ambaye amefikisha mabao sita kwenye ligi ameifungia timu yake bao la ushindi dakika ya 79 kwa mkwaju wa penalti kufuatia beki wa Geita Gold, Kelvin Yondani kunawa mpira katika harakati za kuokoa hatari langoni mwao.

Mbrazil huyo amefunga bao hilo akiwa ametoka kuifungia bao pekee lililowapa ushindi ugenini dhidi ya Dodoma Jiji ila leo alipofunga alifunua jezi na kuonekana ujumbe wa kumuenzi gwiji huyo wa soka ulimwenguni aliyefariki dunia jana.

Bao lingine la Singida Big Stars limefungwa na beki Mkongomani, Biemes Carno dakika ya 30 akimalizia krosi ya Deus Kaseke, bao hilo ni la kwanza kwa beki huyo tangu ajiunge na Singida BS msimu huu.

Deus Kaseke amefikisha asissti nne msimu huu sawa na Nicolas Gyan, huku Rodrigo Fegu na Amis Tambwe wakiwa na assisti mbili kila mmoja, wakati Meddie Kagere, Bruno Gomes, Peterson Cruz, Paul Godfrey na Said Ndemla wakitoa pasi moja ya bao.

Geita Gold imepata bao lake kupitia kwa beki, Haruna Shamte kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 45 baada ya mshambuliaji wa timu hiyo, Juma Luizio kuangushwa katika eneo la hatari akielekea kufunga bao.

Mtanange huo ambao umechezwa kuanzia saa 10:02 jioni ni wa pili kwa timu hizo kukutana katika ligi, ambapo katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Septemba 27, 2022 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ulimalizika kwa sare ya 1-1.

Baada ya kuruhusu mabao mawili leo, Kipa wa Geita Gold, Sebusebu Samson amepata cleensheet (kutoruhusu bao) moja pekee katika mechi tisa za ligi alizodaka msimu huu, akiruhusu mabao 13 ambapo cleensheet nyingine aliipata kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Transit Camp.

Singida Big Stars imepoteza mchezo mmoja tu nyumbani Uwanja wa Liti, Singida dhidi ya Coastal Union, ikicheza mechi 10 kushinda saba na sare mbili.

Kichapo hicho kinaifanya Geita Gold ipoteze mchezo wa tatu ugenini msimu huu ikifungwa na Simba, Dodoma Jiji na Singida Big Stars, ambapo imecheza mechi 10 ikishinda tatu dhidi ya Polisi Tanzania, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons na sare nne mbele ya Kagera Sugar, Azam, Coastal Union na Mbeya City.

Nyota wapya wa Singida Big Stars, Ibrahim Ajibu na Nassoro Saadun wamecheza kwa mara ya kwanza tangu wajiunge na timu hiyo kwenye dirisha dogo la usajili, ambapo Ajibu ameingida dakika ya 62 kuchukua nafasi ya Deus Kaseke huku Saadun akiingia badala ya Meddie Kagere dakika ya 87.

Singida Big Stars imefikisha pointi 37 ikijiimarisha katika nafasi ya nne huku Geita Gold ikibaki kwenye nafasi ya saba ikiwa na pointi 24.