Singida, Prisons zafungiwa kusajili

Muktasari:

  • KLABU za Tanzania Prisons na Singida Big Stars zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, zimepigwa rungu la kutofanya usajili kwa kipindi cha dirisha moja huku makipa Mussa Mbissa na Metacha Mnata wakiwa chanzo.

KLABU za Tanzania Prisons na Singida Big Stars zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, zimepigwa rungu la kutofanya usajili kwa kipindi cha dirisha moja huku makipa Mussa Mbissa na Metacha Mnata wakiwa chanzo.

Taarifa ya kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu iliyotoka leo Oktoba 7, 2022 imeeleza timu hizo zimefungiwa kutokana na kufanya usajili wa wachezaji hao ilihali wakiwa na mikataba na klabu zao za awali.

Taarifa hiyo imeeleza, Singida ilimsajili Metacha huku akiwa bado na mkataba na Polisi Tanzania hivyo hivyo kwa Prisons iloyomsajili Mbisa huku akiwa bado na mkataba na Coastal Union.

Kwa mujibu wa kamati hiyo, uamuzi huo umezingatia kanuni ya 47 (21) ya Ligi Kuu.

Hata hivyo, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imezikumbusha klabu zote nchini kuwa ussjili wa wachezaji unafanywa kwa kuzingatia kanuni na timu ambazo zitakiuka kanuni hizo, zitachukuliwa hatua.

Katika matoleo ya gazeti hili kipindi cha usajili mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu liliripoti kuwepo na utata katika sakata la usajili wa wachezaji hao.