Singida Big Stars yatuma salamu Ligi Kuu

TIMU ya Singida Big Stars imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Zanaco FC ya Zambia katika mchezo wa kirafiki uliopigwa leo mkoani Singida.

Big Stars imepata ushindi huo leo Alhamisi katika mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa ambao umechezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida katika tamasha la Singida Big Day.

Ushindi huo ni kama Singida Big Stars ambayo imepanda daraja msimu huu imetuma salamu Ligi Kuu kwa wapinzani wake katika michuano hiyo ambayo itaanza Agosti 15.

Bao pekee katika mchezo huo limefungwa na Deus Kaseke mnamo dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza kwa shuti kali baada ya walinzi wa Zanaco kushindwa kuondoa mpira wa krosi uliopigwa na Amissi Tambwe.

Bao hilo limedumu kwa dakika 45 za kwanza na kuipelekea Singida Big Stars mapumziko ikiongoza 1-0, huku kipindi cha pili wageni Zanaco wakiuanza mchezo kwa nguvu na kutafuta bao la mapema la kusawazisha.

Juhudi zao zimegonga mwamba kufuatia washambuliaji wake kukosa umakini katika eneo la mwisho huku mabeki wa Singida wakiongozwa na Paschal Wawa wakicheza vyema na kuzima mashambulizi hayo.

Benchi la ufundi la Singida Big Stars limefanya mabadiliko ya wachezaji wanne katika kipindi cha pili likiwatoa Amissi Tambwe, Shafiq Batambuze, Joao Gomez na Peterson Cruz huku nafasi zao zikichukuliwa na Kelvin Sabatho, Nicolas Gyan, Yassin Mustapha na Oliveira.

Mabadiliko hayo yameleta uhai kwenye kikosi hicho na kutawala mchezo katika dakika 10 za mwisho wakitengeneza nafasi za mabao na kupiga soka la kuvutia, lakini milango ikaendelea kuwa migumu na kufanya bao pekee lililofungwa na Deus Kaseke kudumu kwa dakika 90 za mchezo huo.

Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi ya kikosi cha Singida ambacho kimepanda Ligi Kuu Bara msimu huu kikitarajia kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Agosti 16 nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons.

Kikosi cha Singida Big Stars kilichoanza kwenye mchezo huo ni Benedict Haule, Juma Abdul, Shafik Batambuze, Paschal Wawa, Biemes Corno, Deus Kaseke, Said Ndemla, Peterson Cruz, Amissi Tambwe na Dario Frederico.