Simba yawaduwaza Watswana

Sunday October 17 2021
simbaaa pic
By Daudi Elibahati

KLABU ya Simba imenza vyema michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Simba ilianza kupata bao la kwanza dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa kiungo wake Mganda, Taddeo Lwanga aliyepiga shuti kali baada ya mpira wa kona uliopigwa na Rally Bwalya kuzama kwenye eneo la 18 la Galaxy.

Wakati Galaxy wakiendelea kutafakari jinsi walivyofungwa bao la mapema iliwachukua Simba dakika ya sita ya mchezo kuandika bao la pili lililofungwa na nahodha wa timu hiyo John Bocco.

Bao hilo halitofautiani sana na lile la kwanza kwani lilitokana na kona fupi iliyopigwa na winga Bernard Morrison kwa kiungo Bwalya ambaye alipiga krosi safi kwenye eneo la hatari la Galaxy na nyota huyo kufunga kwa shuti kali.

Baada ya mabao hayo mawili ya mapema, Galaxy walianza kutafuta mabao ya kusawazisha lakini walijikuta wakikwama kwenye ukuta wa Simba uliokuwa unalindwa vizuri na mabeki wa kati Pascal Wawa na Henoc Inonga Baka 'Varane'.

Matokeo hayo yanakuwa na faida kubwa kwa Simba kwani Jwaneng watakuwa na kibarua kizito cha kupindua matokeo wakati watakapokuja kwenye mchezo wa marudiano utakaofanyika Octoba 24, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Advertisement

Simba wanahitaji sare au ushindi wa aina yeyote ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwa na kumbukumbu ya kuishia hatua ya robo fainali msimu uliopita.

Advertisement