Simba yatakata kwa Mkapa…Huyo Morrison mh!

Simba yatakata kwa Mkapa…Huyo Morrison mmhh!

Muktasari:

  • Klabu ya Simba imetumia vyema uwanja wa nyumbani na kufanikiwa kuifunga Red Arrows ya Zambia mabao 3-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika

DAKIKA 90, zimekamilika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Red Arrows katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabao mawili ya Bernard Morrison dakika ya 17, 78, na Meddie Kagere dakika ya 19, yametosha kuipa ushindi mnono mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ambapo Simba ilimtoa beki Pascal Wawa na nafasi yake ikichukuliwa na Henock Inonga ili kuiongezea nguvu safu ya ulinzi.

Kwa upande wa Red Arrow ilifanya mabadiliko kwenye eneo la ushambuliaji akitoka Felix Bulaya na nafasi yake ikichukuliwa na Ricky Banda.

Kuingia kwa Inonga kulileta utulivu kwenye eneo hilo kutokana na urefu wake wa kucheza mipira mingi ya kichwa ambayo ilikuwa inatumika kama njia mbadala ya kutafuta mabao.

Dakika ya 57, Prosper Chiluya wa Red Arrows alipata kadi nyekundu baada ya kadi mbili za njano na kuendelea kuigharimu timu yake iliyokuwa  ikihitaji kusawazisha mabao hayo.

Dakika ya 72, Kocha wa Simba Pablo Franco alifanya mabadiliko kwenye eneo la kiungo akiwatoa Hassan Dilunga na Sadio Kanoute na nafasi zao zikichukuliwa na Ibrahim Ajibu na Mzamiru Yassin.

Dakika ya 78, Simba ilipata bao la tatu kupitia kwa Bernard Morrison na kufikisha mabao mawili katika mchezo wa leo baada ya mabeki wa Red Arrows kuzembea katika eneo la hatari.

Simba ilifanya mabadiliko mawili ya mwisho baada ya kumtoa mfungaji wa bao la pili Meddie Kagere nafasi yake ikichukuliwa na John Bocco huku akitoka Larry Bwalya nafasi yake ikichukuliwa na Peter Banda.

Simba wameangukia michuano hii baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa bao la ugenini baada ya kufungana mabao 3-3, huku kwa upande wa Red Arrows wakifika hatua hii baada ya kuitoa Klabu ya C. D. Primeiro de Agosto ya Angola kwa jumla ya bao 1-0.

Huu ni ushindi wa kwanza wa michuano ya kimataifa kwa kocha Pablo Franco tangu kuteuliwa kukinoa kikosi hicho huku ukiwa wa pili wa mashindano baada ya ule wa Ligi Kuu NBC wa mabao 3-1, dhidi ya Ruvu Shooting Novemba 19 katika Uwanja wa CCM kirumba.

Timu hizo zitarudiana tena Disemba 5, nchini Lusaka Zambia na mshindi wa jumla atatinga moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ya michuano hii.