Simba yarejea kibabe Dar, wapewa ruhusa siku moja

Thursday August 04 2022
DAR PIC
By Eliya Solomon

KIKOSI cha Simba, kimerejea nchini leo, Alhamisi Julai 4 mchana na Shirika la ndege la Ethiopia kikitokea Misri ambako kiliweka kambi tangu Julai 15 kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara 2022/23.

Ikiwa Misri chini ya benchi jipya la ufundi linaloongozwa na Mserbia,  Zoran Manojlovic kwenye mji wa Ismailia, Simba ilicheza michezo minne ya kirafiki, ilishinda miwili, sare moja huku ikipoteza mara moja.

Mchezaji wa kwanza kutoka nje ya uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere alikuwa ni kipa chaguo la tatu, Ally Salim akifuatiwa na Beno Kakolanya huku wengine wakifuata mmoja mmoja.

Licha ya kuwepo kwa Basi la klabu uwanjani hapo wachezaji walionekana kutawanyika huku wachache wakiingia kwenye usafiri huo wa timu.

Mwanaspoti ilifuatilia na kubaini kuwa wachezaji hao wamepata ruhusa ya siku moja kabla ya kesho kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na kilele cha tamasha lao, Agosti 8.

Wakati ikisubiriwa kumwona Zoran akitokeza ilikuwa tofafauti kwani ilichukua zaidi ya lisaa hakuonekana sambamba na meneja wa timu, Patrick Rweyemamu.

Advertisement

Ndipo ilipoanza minong'ono kuwa pengine wamekwama ndani wakati wa ukaguzi pamoja na wachezaji wengine ambao awali hawakuonekana.

Simba ilianza  kucheza mchezo wake wa kirafiki dhidi ya dhidi Ismaily na kuambulia sare ya bao 1-1 kisha wakacheza dhidi ya Abou Hamad na kufanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6–0, huku mchezo wa tatu wakipoteza kwa mabao 2–0 dhidi ya Haras El Hodoud.

Mchezo wa mwisho wa kirafiki ulikuwa dhidi ya Al Kholood inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Saudi Arabia ambapo waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Msimu uliopita ambao Simba ilishika nafasi ya pili ilienda Morocco kujiandaa na kampeni za 2021/22, walicheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya FAR Rabat (2-2) na dhidi ya Olympique (1-1).

Advertisement