Simba yapangua fitna

Simba yapangua fitna

Muktasari:

WACHEZAJI 24 wa kikosi cha Simba na benchi la ufundi jana mchana waliwasili salama kwenye mji wa Jos, Nigeria, lakini mashushushu wa Wekundu hao wameshtukia na kupangua fitna kadhaa.

WACHEZAJI 24 wa kikosi cha Simba na benchi la ufundi jana mchana waliwasili salama kwenye mji wa Jos, Nigeria, lakini mashushushu wa Wekundu hao wameshtukia na kupangua fitna kadhaa.

Fitna ya kwanza ilikuwa ni ugumu wa kupata ndege ya kusafirisha wachezaji wao kutoka Abuja kwenda Jos, lakini Simba ambao waliwahi mjini hapo wakapambana kiume mpaka kupata ndege ya kusafirisha mastaa wao na baadhi ya viongozi wakasafiri kwa basi. Plateau walibaki wameduwaa kwani Simba imepangua fitna hiyo na wachezaji walitua kambini kwa wakati wakiwa na mzuka.

Mmoja wa viongozi wa Simba aliiambia Mwanaspoti kwamba mashushushu wao wamewadokeza kwamba kuna mpango wenyeji wao wameusuka wa kuwabambikia maambukizi feki ya corona mastaa wa Simba akiwemo Luis Jose, Clatous Chama na John Bocco ili wasicheze mechi hiyo muhimu ya kesho. “Tumegundua kwamba wanataka kuwabambikizia maambukizi feki ili wasicheze, lakini sisi tumeshagundua na tunapambana nao. Wamepanga pia mechi isiwe laivu ili wafanye hujuma zao, lakini hata wamepanga kuwawekea na mizengwe wapishi wa timu yetu,” alidokeza kiongozi wa Simba na kusisitiza kuwa kila kitu watakiweka sawa.


KAMBINI JOS

Tayari Simba iko kambini kwa mchezo huo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United uliopangwa kufanyika kesho kuanzia saa 12.00 jioni.

Wachezaji hao waliwasili wakiwa na morali kubwa kuelekea mchezo huo na leo kuanzia saa 10.00 jioni watafanya mazoezi yao kwenye uwanja wa New Jos ambao utatumika katika mechi hiyo ambayo serikali imetangaza hautakuwa na mashabiki.

Kikosi cha Simba kilitumia saa moja kusafiri kwa ndege kutua Jos, huku baadhi ya viongozi wakiwa wametangulia mapema kwa lengo la kukamilisha maandalizi na kudhibiti fitna. Viongozi hao walikuwa na jukumu la kuhakikisha wachezaji wao wanafikia katika hoteli nzuri na yenye usalama wa hali ya juu ili kujilinda na aina yoyote ya hujuma ikiwemo walizotaja hapo juu.

Meneja wa timu hiyo, Abbas Selemani alisema kuwa mpaka jana jioni hakuna majeruhi yeyote katika kikosi chao na wachezaji wana morali ya hali ya juu, huku akiwahakikishia mashabiki kwamba mambo ni mazuri.

Selemani alisema kuwa wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya mchezo huo ambao mpaka sasa umekuwa gumzo kubwa nchini humo.

“Kwa kifupi, hakuna majeruhi na wachezaji wana morali ya hali ya juu, tupo tayari kwa mechi,” alisema Selemani huku akidokeza kwamba mechi hiyo imekuwa gumzo kwenye mitaa ya Nigeria kwani walishazoea mechi nyingi kuanzia ugenini.

Na THOBIAS SEBASTIAN