Simba yaongoza dakika 45

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza zilianza kwa timu zote kucheza kwa tahadhari huku zikishambulia kwa kushtukiza.

Mchezo huo uliendelea huku Ahly wakionekana kucheza kwa kujiamini zaidi ya Simba walikuwa nyumbani na dakika ya 30  kupitia kwa Luis Miquissone Simba walipata bao la kuongoza.

Baada ya bao hilo mechi iliendelea kuwa ya utulivu kwa timu zote mbili Al ahly wakimdhibiti kwa umakini mshambuliaji wa Simba Chriss Mugalu huku beki wa Simba Paschal Wawa na Joash Onyango wakikabiliana kiufundi na mshambuliaji wa Ahly, Walter Bwalya.

Mchezo uliendelea kuwa wa kutegeana namna hiyo mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika na Simba kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya vigogo hao wa Afrika.

Timu zote mbili katika kipindi cha kwanza zilitengeneza zaidi ya nafasi mbili za kufunga mabazo hazijazaa mabao katika dakika 45 hizo zilizomalizika Simba wakiongoza.


MASHABIKI SHANGWE

Uwanja wa Benjamin Mkapa, unasikika kwa shangwe, kuzomea, ngoma, vuvuzela na makofi, ambapo Simba inacheza na Al Ahly ya Misri.
Mechi hiyo ni ya pili kwa  Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,baada ya kushinda ugenini na AS Vita bao 1-0.

Shangwe hilo linatokana na timu hiyo kuongoza bao 1-0 kipindi cha kwanza, lililofungwa na Miquissone.

Wakati kelele za kuzomea zilizosikika kwa mashabiki wa Simba, ilitokana na wachezaji wa Al Ahly wakikwamishwa na mabeki kufika langoni aliposimama Aishi Manula.

Mbali na mashabiki kuwajibika kwa upande wao, hali halisi viti vya mzunguko vya kijani watu wapo wachache, huku baadhi ya watu wakiwa nje kusubili utaratibu wa kuingia.
Kwa upande wa askari nao wapo makini na kazi yao ya kusimamia mashabiki waliopo ndani kuhakikisha kila mmoja anafuata taratibu ya kukaa sehemu anayotakiwa.