Simba yamkana Manara

Simba yamkana Manara

BAADA ya Ofisa habari wa Simba, Haji Manara kutoa kauli iliyoashiria ubaguzi wa mashabiki kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya Plateau United ya Nigeria ,klabu yake imetoa tamko juu ya kauli hizo.

Simba itaikaribisha Plateau United Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa katika mchezo wa marudiano raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya mchezo wa kwanza wekundu wa Msimbazi kushinda bao 1-0 ugenini.  

Katika mkutano wa waadnishi wa habari uliofanyika jana Jumatano,Manara alinukuliwa akisema "Kwenye mchezo wa Jumamosi pale kwa Mkapa hatutaruhusu mashabiki wa upande wa pili kuingia na jezi zao za njano.Hii mechi ni yetu na tunataka hizo asilimia 30 za mashabiki watakaoruhusiwa kuingia uwanjani wawe wa Simba tu," alisema Manara.

Kauli hio imepigwa vikali na wadau wa soka nchini likiwemo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambao wameeleza kuwa ni haki ya kila shabiki kuingia uwanjani kutizama mechi yeyote bila kujali upande wake na hiyo ni kutokana na kanuni za shirikisho la mpira duniani FIFA.

Hata hivyo leo Alhamis kupitia mtandao wao kijamii wa Instagram, Simba wamekanusha kutomtuma Haji Manara kutoa kauli hiyo na kuahidi kumpa adhabu ama onyo kulingana na kanuni za ndani ya klabu hiyo.

"Klabu ya Simba inapenda kuutarifu umma kwamba kauli inayoashiria kuzuia baadhi ya washabiki wasifike uwanjani kuangalia mchezo kati ya Simba na Plateau ya Nigeria haikutolewa kwa maelekezo ya klabu,"  

"Klabu imechukua hatua za kiutawala za ndani ya klabu kuhakikisha kwamba suala kama hili halitokei tena,"ilisomeka taarifa hiyo.