Simba yalamba dili jingine

Muktasari:

Wiki iliyopita Simba walisani mkataba na Air Tanzania wenye thamani ya zaidi Milioni 400.

KLABU ya Simba imepata dili jingine baada ya kusaini mkataba wa zaidi ya milioni 300 na kampuni ya Emirate Aluminium ACP.

Simba imesaini mkataba huo wa miaka miwili leo Jumanne katika ofisi za kampuni hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema uwepo wa Aluminium katika timu yao unaongeza chachu ya wachezaji kufanya vizuri.

“Tumesaini mkataba wa miaka miwili lengo likiwa ni kuwapa motisha  wachezaji wetu kwa kila mwezi ili waendelee kupambana,” amesema Barbara.

Barbara amesema kampuni hiyo imeamua kuweka pesa baada ya kuona faida ambayo wameipata katika msimu uliopita.

“Awali tulianza kwa kuwaangalia kwa miezi kadhaa, walikuja na kusema wanataka kutoa tuzo kwa ajili ya mchezaji bora wa kila mwezi na baadae kipa na mchezaji bora wa mwaka,” amesema Barbara.

Naye mkurugenzi wa Emirate Aluminium ACP, Deogratius Marandu amesema wameendeleza ndoto yao ya kufanya kazi na Simba.

“Tuna ndoto na Simba na imechangia kuendelea kudhamini tuzo za wachezaji bora wa mwezi kwenye klabu hii,” amesema Marandu.