Simba yafia kwa Maafande Mbeya

Sunday June 26 2022
simbaa pic
By Daudi Elibahati

TIMU ya Tanzania Prisons imetumia vyema Uwanja wake wa Sokoine baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Bao la Prisons limefungwa na beki wake Benjamin Asukile dakika ya 54 baada ya piga nikupige kwenye lango la Simba na kumshinda kipa Beno Kakolanya.

Matokeo haya yanakuwa na faida zaidi kwa Prisons kwani baada ya mchezo huo inasogea hadi nafasi ya 14 na pointi 29 na kuishuka Biashara United iliyopo ya 15 na pointi 28 baada ya timu zote kucheza michezo 29.

Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Prisons dhidi ya Simba ikiwa nyumbani kwani mara ya mwisho waliokutana katika Uwanja wa Nelson Mandela Oktoba 22, 2020 ilishinda pia bao 1-0.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza uliozikutanisha timu hizi Februari 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ilishinda bao 1-0.

Huu unakuwa ni mchezo wa tatu kwa Simba kupoteza baada ya kufungwa bao 1-0 na Mbeya City Januari 17 na Kagera Sugar Januari 26, mwaka huu.

Advertisement

Katika mechi zilizosalia kwa Tanzania Prisons ni dhidi ya Ruvu Shooting Juni 29, kwenye Uwanja wa Mabatini wakati Simba itamenyana na Mbeya Kwanza iliyoshuka daraja katika Uwanja wa Majimaji Songea.

Advertisement