Simba yaanza na sare, Bocco akosa penalti

MCHEZO wa Ligi Kuu kati ya Biashara United na Simba umemalizika kwa suluhu ya 0-0 ikiwa ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2021/2022 kwa timu zote mbili.
Dakika 45, za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa suluhu na huku kikionekana kuwa kigumu kwa timu zote mbili na kuwalazimu kushambuliana kwa kushitukiza.

Kipindi cha pili Biashara iliongeza nguvu kwa kumuingiza Stephen Ziga kwenye eneo la Ushambuliaji na Simba kufanya mabadiliko kwa kuwa Mohammed Hussein  na Dancun Nyoni walioingia kuchukua nafasi za Kapombe na Bwalya.

Mabadiliko hayo kwa timu zote mbili yaliomekana kuleta mabadililo na dakika ya 55, Ziga alipiga kiki ya chini chini iliyokwenda nje ya lango la Simba.

Simba iliendelea kufanya mabadiliko dakika ya 58 kwa kuwatoa Inonga na Dilunga na nafasi zao kuchukuliwa na Peter Banda na Yusuph Muhilu walioingia kuongeza mashambulizi langoni kwa Biashara.

Kassim Mdoe na Ambrose Levocatus Kazilahabi waliingia kwa upande wa Biashara na kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji akitoka Denis Nkane na Ramadhan Chombo na kuipa uhai Biashara kwenye safu ya  mbele.

Lango la Biashara liliendelea kushambuliwa na Simba na dakika ya 68 Nyoni kidogo aipatie  bao la kuongoza baada ya kuanzishiwa mpira harakaharaka na Duncan    lakini akapiga shuti lililopaa juu ya goli la Biashara.

74 Banda alikosa bao baada ya kupiga shuti lililoenda nje kidogo ya lango la Biashara na dakika nne baadae biashara walilipa mashambulizi kupitia kwa Kazilahabi aliyepiga tikitaka na kudakwa na Manula.

Dakika 84 Kagere alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Pape Sakho na muda huo huo Biashara ilimiliki mpira hadi dakika ya 86 walipopokonywa.

Dakika ya 87, Biashara ilipoteza nafasi ya bao na muda huo huo Sakho wa Simba akakosa bao kwa kupiga mpira ulioenda nje.

Dakika ya 89, Sakho alichezewa faulo faulo ndani ya enei la 18 la Biashara na refa kuamulu ipigwe penalti iliyopigwa na Bocco na kuokolewa na kipa wa Biashara Ssetuba.