Simba waanika sakata la Lwanga, Morrison ndani
Baada ya sakata la kiungo mkabaji wa Simba, Taddeo Lwanga kutoonekana jina lake kwenye usajili wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amemaliza utata wa sakata hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 22, 2020 jijini Dar es Salaam Gonzalez amesema wameshamaliza taratibu zote za usajili an anavibali kucheza Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Lwanga alisajiliwa siku nyingi na anavibali vyote vya kucheza Ligi Kuu Bara, Ligi ya mabingwa na mashindano mengine yote," amesema Barbara
Gonzalez amezungumzia pia kutoonekana kwa nyota wao Bernard Morrison kwenye michezo kadhaa ni kutokana na kusumbuliwa na majeraha na sasa ameshapona hivyo atashiriki kwenye Simba Super Cup kuanzia Januari 27.
"Morrison alikosekana katika baadhi ya michezo kutokana na majeraha lakini kwa sasa amepona na anaendelea vizuri na ataingia kambini na atakuwepo katika mashindano yetu," amesema Gonzalez