Simba Queens wako fiti, Simba SC wavurugwa

Muktasari:

  • Timu za Simba (Wanawake na Wanaume) ziko jijini Mwanza, ambapo Simba Queens wanakipiga kesho na Alliance Girls na Simba SC watakuwa kibaruani Jumamosi kukichafua na Gwambina huko wilayani Misungwi.

Mwanza. Wakati vinara wa Ligi Kuu ya Wanawake, Simba Queens wakijirusha uwanjani kesho Ijumaa Aprili 23, 2021 kuwavaa Alliance Girls, Nahodha wa timu hiyo Vaileth Nicholous amesema wako tayari kwa mchezo huo kusaka alama tatu ili kuendelea kujiweka pazuri kwenye mbio za ubingwa.

Simba Queens ndio wanaongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 39 wakiwaacha watani zao, Yanga Princess alama moja na kesho watakuwa kazini dhidi ya Alliance Girls mchezo utakaopigwa uwanja wa Nyamagana jijini hapa.

Wakati timu hizo zikikutana, Simba Queens wanakumbukumbu ya ushindi wa mabao 4-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa jijini Dar es Salaam, hivyo kesho ni kisasi au kuendeleza ubabe.

Akizungumza na Mwanaspoti Online baada ya mazoezi yao ya leo Alhamisi, Vaileth amesema wako fiti na maandalizi waliyoyafanya yanatosha kuondoka na ushindi.

"Tunahitaji ushindi kwa sababu malengo yetu ni kutetea ubingwa msimu huu, tunafahamu mechi itakuwa ngumu ila tumejipanga kupata matokeo mazuri" amesema Nahodha huyo.

Wakati huohuo, kikosi cha Simba kwa upande wa wanaume, tayari kimewasili jijini Mwanza kikitokea mjini Bukoba kilipokuwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar na kushinda mabao 2-0.

Taarifa za awali ilizopata Mwanaspoti, Wekundu hao, walikuwa wafanye mazoezi yake kwenye uwanja wa CCM Kirumba lakini imeelezwa kuwa ratiba zimevurugika.

Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu amesema ratiba yao ilikuwa wajifue kwa ajili ya mechi dhidi ya Gwambina lakini kuchelewa kwa timu hiyo kumevuruga kila kitu.

"Tumechelewa kufika Mwanza kwahiyo ratiba zimevurugika, tulihitaji kufanya mazoezi leo jioni ila imeshindikana na hadi kesho Ijumaa tutajua program za Kocha, siunajua tuna mechi Jumamosi na Gwambina.." amesema Rweyemamu.