Simba: Njooni mhesabu

MASHABIKI wa soka wa Jiji la Mbeya leo watapata burudani kwenye Uwanja wa Sokoine, Simba itakuwa wageni wa Tanzania Prisons.

Mechi hiyo ina mambo mawili, kisasi na mbio za kuepuka kushuka daraja kwa maafande ambao watakuwa wakitaka kulipa kisasi cha kichapo cha bao 1-0 walichopewa katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam.

Katika mechi yao ya mwisho ya nyumbani kwa Prisons msimu uliopita Sumbawanga, Rukwa, Simba ilicharazwa bao 1-0, hivyo kulifanya pambano hilo kuwa gumu.

Simba chini ya Seleman Matola imeshajihakikishia kumaliza nafasi ya pili katika msimamo, lakini inasaka ushindi ili kuwapa faraja mashabiki wake kwa kupata ushindi utakaowafuta machozi ya kumaliza msimu pasipo kutwaa taji la Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na lile la Shirikisho la Azam (ASFC).

Katika mechi tatu mfululizo Simba ikiwa na Matola imeshinda zote ikifunga mabao manane na kuruhusu moja tu, ikiifunga Mbeya City 3-0, kuinyoa KMC 3-1 na kisha kuichakaza Mtibwa 2-0 na mashabiki wa timu hiyo wanaamini hata leo wataendelea kuhesabu mabao mbele ya Prisons.

Prisons ina kibarua wakilazimika kupata pointi tatu leo ili wajiweke katika mazingira mazuri ya kuepuka kushuka daraja, kwani ushindi utawafanya wafikishe pointi 29 zitakazowaweka katika uwezekano mkubwa wa kuepuka kushuka daraja moja kwa moja.

Nyota watatu wa Simba, Meddie Kagere, Kibu Denis na Pape Sakho watakuwa katika mpambano baina yao ambao ni ule wa kusaka heshima ya kumaliza akiwa mfungaji bora wa timu hiyo.

Wakati Kibu Denis akiwa kinara hadi sasa na mabao manane, Kagere anashika nafasi ya pili akiwa na mabao saba wakati Sakho yuko nafasi ya tatu na mabao sita.

Mwendelezo wa kupata matokeo mazuri na kiwango bora cha kuvutia cha Simba ambacho kimeonekana katika mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City, KMC na Mtibwa Sugar ni swali gumu ambalo kaimu kocha mkuu wa Simba, Seleman Matola bila shaka anaifanya Prisons ijiulize na kutafutia majibu katika mechi ya leo.

Matola ameifanya Simba iwe na balansi nzuri katika kila idara na kudhihirisha hilo, katika mechi hizo tatu imefunga mabao manane na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.

Ni mechi ya kitanzi kwa baadhi ya nyota wa Simba ambao mikataba yao imefikia ukingoni na wale ambao wamesotea benchi au kutoonyesha kiwango kizuri msimu huu wanaohitajika kucheza vyema ili kulinda nafasi zao kikosini msimu ujao.

Makocha wa timu hizo, Patrick Odhiambo wa Tanzania Prisons na Matola kwa upande wa Simba kila mmoja ametamba kusaka ushindi leo.

“Hatupo katika nafasi nzuri hivyo tunahitajika kupata ushindi dhidi ya Simba ili tuongeze pointi ambazo zinaweza kutusaidia tuepuke kushuka daraja.”

“Tunakutana na Simba ambayo ni timu kubwa na imekuwa ikifanya vizuri hivyo mechi itakuwa ngumu lakini naamini kama wachezaji watafuata kile tulichowaelekeza, tutafanya vizuri,” alisema Odhiambo.

Matola aliendelea kusisitiza kuwa wanataka kumaliza vizuri msimu.

“Tanzania Prisons ni timu nzuri na mara nyingi tunapokutana nao, mechi huwa ngumu hivyo hata hii tunaamini haiwezi kuwa rahisi ukizingatia pia wanapigania kubaki kwenye ligi.”