Simba: Ngoja tuwaoneshe, yasema ina sapraizi

MASHABIKI wa Simba wamesikia tambo za watani wao, Yanga baada ya kufanya tamasha lao la Wiki ya Mwananchi, kisha wakacheka sana na kuwaambia wenye matamasha yao sasa ndio watawaonyesha kitu gani huwa kinafanyika kwenye matamasha kama hayo.

Kama hujui Simba leo Jumatatu ina tamasha lake la Simba Day linalofanyika kwa msimu wa 13 na baadhi ya mashabiki wa Simba wamewatambia wenzao kwa kuwaambia ‘si mlishindwa kuujaza uwanja, sisi tunaujaza...si mlishindwa kuifunga timu mliyoialika, sisi tunawaonyesha namna ya kuhitimisha tamasha kijanja.’

Kutokana na mashabiki hao, kilele cha Tamasha la Simba Day leo Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam ni mtoko wa kipekee uliobeba historia ya aina yake inayowafanya watembee kifua mbele mbele ya mashabiki wa timu nyingine nchini.

Ni tukio linalothibitisha ujasiri na uthubutu ulioifanya klabu hiyo kuwa muasisi wa wa matamasha ya soka kwa klabu hapa nchini katika kipindi kama hiki kwa ajili ya utambulisho wa vikosi vyao ambavyo vinatumika kwa msimu unaofuata.

Leo ni kilele cha Simba Day, tamasha lililoasisiwa mwaka 2009 chini ya uongozi wa aliyekuwa mwenyekiti wa Simba wakati huo, Hassan Dalali ‘Field Marshall’ na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda.

Baada ya maandalizi ya wiki tatu huko Misri katika Jiji la Ismailia, kikosi cha Simba kinaonekana kuwa tayari kwa ajili ya ushindani wa msimu ujao katika mashindano tofauti kitakachoshiriki yale ya ndani na ya kimataifa lakini pia kupigania mataji ya Ligi Kuu ya NBC, Ngao ya Jamii na Azam Sports Fedaraion Cup (ASFC) ambayo iliyapoteza msimu uliopita.


SAPRAIZI YA MASTAA

Hamu ya kuona kitu gani timu hiyo imekivuna huko Misri ndicho kilichopo kwa mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba pamoja na wadau wa soka nchini lakini zaidi ni kwa nyota saba ambao timu hiyo imewanasa katika dirisha kubwa la usajili linaloendelea.

Augustine Okrah, Nelson Okwa, Mohamed Ouattara, Moses Phiri, Victor Akpan, Habib Kyombo, Nassor Kapama na Dejan Georgjevic ambao huenda wakaonekana kwa mara ya kwanza wakivalia jezi ya Simba ndani ya ardhi ya Tanzania.

Straika Mserbia, Georgijevic aliyekuwa akikipiga NK Domzale ya Ligi Kuu ya Slovania, aliyewahi kucheza pia Serbia, Hungary, Kazakhstan na Bosnia& Herzegovina ametambulishwa jana Jumapili.

Muunganiko wa nyota hao na wale ambao walikuwepo kikosini hapana shaka ni jambo linalosubiriwa na wengi ili kupima utayari wa kikosi hicho ambacho kwa sasa kipo chini ya Kocha Zoran Maki kutoka Serbia.

Kocha huyo alisema Timu ya St. George ambayo watakabiliana nayo ni kipimo tosha kwao kwa majukumu yaliyo mbele yao.

St George ilitua juzi na jana ilijifua kujiweka tayari kwa pambano hilo ambalo litakuwa ni la tano la wenyeji tangu iwe chini na Kocha Zoran Maki.

“Tulikuwa na kambi nzuri Misri ambayo imetupa maandalizi mazuri kwa ajili ya msimu unaofuata. Nafurahi kupata mechi hii ya kirafiki ambayo itatupa fursa ya kuonyesha namna tulivyojiandaa na mashindano yaliyo mbele yetu,” alisema Maki.


MOTSEPE ANUKIA

Taarifa ambazo hazijathibitishwa na uongozi wa Simba inaripoti kuwa Simba imewasilisha ombi maalum kwa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Patrice Motsepe ili awe mgeni rasmi katika tukio hilo la leo.

Tetesi za ombi la Simba kwa Motsepe zilikolezwa jana na Rais a Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia jana.

“Nimesikia Simba nao wamemualika Rais wa Caf lakini sina uhakika kama tayari amethibitisha kuwepo kwake,” alinukuliwa Karia Ijumaa iliyopita.


MAANDALIZI KABAMBE

Kwa mujibu wa meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, Mandalizi ya kilele cha tamasha la Simba Day leo yamekamilika huku akitoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi.

“Maandalizi yameenda vizuri na kwa zaidi ya asilimia 99 yamekamilika. Tumejipanga vilivyo kuhakikisha Wanasimba na Watanzania ujumla hawajutii kuja uwanjani siku ya kilele cha Simba Day.”

“Kuna mambo mazuri ambayo tumewaandalia. Iko wazi kwamba Simba ndio wazoefu wa matamasha haya na mashabiki wetu wamekuwa hawatuangushi siku zote. Ninachowasisitiza ni kukata tiketi mapema kwa sababu kasi ya ununuzi wa tiketi imekuwa kubwa wasije kukosa tukio hili kubwa na la kihistoria,” alisema Ally.


VIINGILIO RAFIKI

Katika kuonyesha imedhamiria kuwapa nafasi mashabiki kuhudhuria kwa wingi tamasha hilo, Simba imepanga kiingilio cha chini leo kuwa Sh 5,000 kwa jukwaa la mzunguko.

Bei ya tiketi kwa kiti cha jukwaa la rangi ya machungwa ni Sh 10,000, Sh 20,000 kwa majukwaa ya VIP B&C wakati VIP A ni Shilingi 30,000.

Kwa mujibu wa Ahmed Ally, mageti ya Uwanja wa Benjamin Mkapa yatafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi.


ZUCHU, WHOZU SHOO SHOO

Nyota wa muziki kutoka Kundi la WCB, Zuchu anayetamba na Wimbo wa Fire ndiye atakeyeongoza kundi la wasanii kuburudisha leo.

Mbali na Zuchu, tukio hilo la leo litapambwa pia na Whozu, Meja Kunta na wasanii wengine ambao kwa mujibu wa uongozi wa Simba, watapanda jukwaa kama sapraizi.