Simba: Mziki wetu mnene

Simba: Mziki wetu mnene

SIMBA jana jioni ilikiwasha kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Aigle Noir ya Burundi huku viongozi wakisisitiza sasa mambo yameiva.

Wekundu hao wako Jijini Arusha kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.

Mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mulamu Ng’ambi amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujiandaa kisaikolojia kwenda kuangalia burudani katika kilele cha Simba Day Jumapili Uwanja wa Mkapa.

“Simba Day itakuwa ni kama unaangalia picha ya 3D tukutane kwa Mkapa mapema tu, hakuna shida kuhusu biriani litakuwepo kama kawaida, ila sasa tuna malengo zaidi ambayo uzoefu wataupata kwa kufika uwanjani ikiwa haijawahi kupatikana popote pale,” alisema Mulamu.

Kilele cha Simba Day kimezidi kupamba moto baada wageni wao TP Mazembe kutoa kikosi cha wachezaji 23 watakaotua nchini kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa siku ya kilele hicho Septemba 19.

Nyota Tresor Mputu na Thomas Ulimwengu hawajaorodheshwa kwenye kikosi hicho kitakachowasili Jumamosi, Septemba 18 siku moja kabla ya mechi hiyo. Tamasha hilo litapambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii akiwemo Darasa na Sho Madjozi kutoka Afrika Kusini anayetamba na wimbo wa John Cena.

Viingilio kwenye tamasha hilo ni VIP A 30,000, VIP B&C 20,000 na mzunguko 5,000 na tayari zimeanza kuuzwa kwenye vituo 11.

TP Mazembe ilirejea Jijini Lubumbashi juzi ikitokea Morocco ilipokuwa imeweka kambi na leo wataanza kujinoa kujianda na mechi ya Simba na Jumamosi watatua nchini Tanzania wakiwa na kikosi cha wachezaji 23.

Katika kikosi hicho kuna mziki wote wa Mazembe chini ya benchi jipya lenye uzoefu mkubwa.