Simba mpya tamu!

UONGOZI wa Simba baada ya vikao vya mara kwa mara katika siku za hivi karibuni, umeafikiana kukisuka upya kikosi chao na kuhakikisha mashabiki wake wanakula Sikukuu ya Krismasi wakiwa na furaha na tayari kazi imeanza.

Maamuzi hayo yatakayowagharimu mkwanja mrefu, yamekuja baada ya wote kukubali kukosea kwenye usajili wa dirisha kubwa la msimu huu na sasa wamenza kukifumua na kukijenga kikosi kipya na benchi la ufundi la maangamizi wakianza na maeneo haya;


KOCHA MKUU

Simba tayari imemalizana na kocha Mreno ambaye jina lake halijafahamika hadi sasa kutokana na usiri mkubwa uliopo kwa miamba hiyo ya Kariakoo na kocha huyo anatarajiwa kutua nchini kesho Jumatatu kuanza kazi.

Mreno huyo anakuja Simba kuwa bosi wa Juma Mgunda atakayekuwa msaidizi baada ya kukaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya kuondoka kwa Mserbia Zoran Maki aliyeondoka mwanzoni kabisa mwa msimu huu.

Maamuzi hayo ya Simba kushusha kocha mpya yamekuja ili kumuongezea nguvu Mgunda na timu kuwa na wataalamu wenye mifumo zaidi ya miwili wanayoweza kutumia kwenye mechi tofauti.

Sababu nyingine ya kuleta kocha mpya huyo ni kuongeza mamlaka ya kuheshimika kwa benchi la ufundi kwani Simba imekuwa na wachezaji wengi ambao wana wasifu mkubwa na muda mwingine kushindwa kuheshimu wanachokisema benchi la ufundi.


KOCHA WA MAKIPA

Tayari Simba imeshusha kocha wa makipa wa viwango vya juu Chlouha Zakaria raia wa Morocco mwenye wasifu mkubwa kwenye soka na miongoni mwa timu alizozinoa ni Hassania Agadir ya nchini kwao aliyoifikisha robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (2018-2019) na nusu fainali (2019-2020).

Ujio wa kocha huyo ni kuziba pengo liloachwa na kocha Mohammed Rachid aliyeondoka Septemba 6 mwaka huu na nafasi yake kukaimiwa na Mohamed Mwalami ‘Shilton’ aliyeingia kwenye matatizo hivi karibuni.

Ujio huo wa Zakaria unatarajiwa kuongeza ubora wa makipa wa Simba, Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salim na Ahmed Feruzi.

Tayari kocha huyo ameanza kazi na kuhakikisha makipa hawafanyi makosa kwenye mechi zote wanazocheza na kulifanya lango la Simba kuwa salama zaidi.


KOCHA WA VIUNGO

Baada ya kuondoka kwa Karim Sbai aliyeondoka na Kocha Zoran, Simba ilibaki bila kocha wa viungo kwa zaidi ya miezi miwili kabla ya Alhamis ya wiki hii imemtambulisha M’Afrika Kusini, Kelvin Mandla kushika nafasi hiyo.

Kutokuwa na kocha wa viungo, wachezaji wa Simba walionekana kupata majeraha ya mara kwa mara kutokana na kukosa utimamu wa kutosha wakiwemo, Nelson Okwa, Peter Banda, Jimmyson Mwanuke, Shomary Kapombe, Israel Mwenda na Pape Ousmane Sakho pia wengine kuonekana kuchoka wakati wa mchezo.

Jukumu la kwanza la Mandla litakuwa kuifanya Simba iwe imara na ngangari kama ilivyokuwa misimu iliyopita chini ya Kocha Adel Zrane aliyeondoka.


MTAALAMU WA KUWASOMA WAPINZANI

Licha ya kuwepo mtaalamu wa kusoma na kutathmini ubora na ufanisi wa wachezaji wa Simba sambabana na wapinzani, Mzimbabwe Calvin Mavunga, Simba imeamua kumshusha fundi mwingine kwenye kitengo hicho ili kuongeza nguvu ikiwa ni mapendekezo ya kocha mpya mreno.

Mreno huyo ametaka wenye eneo hilo wawepo wataalamu wawili ili wagawane majukumu na kupata data zoe zinazohitajika ambapo mmoja akiwa anakisoma kikosi cha Simba, mwingine awe anawasoma na kuwatathmini wapinzani ili kurahisisha kazi na kuifanya timu ishinde kila mechi kiurahisi.


MASTAA WAPYA

Mezani kwa Simba tayari kuna majina zaidi ya matano ya mastaa wapya ambao wapo kwenye mipango ya kusajiliwa mapema katika dirisha dogo litakapofunguliwa mwezi ujao.

Katika majina hayo, yamegawanyika kwenye maeneo makuu matatu ambapo kimyakimya Simba inapanga kushusha washambuliaji wa kati wawili wenye makali, kiungo wa ukabaji na beki wa penmbeni mwenye sifa ya kucheza kushoto na kulia kuwasaidia Shomary Kapombe na Mohammed Hussein.

Tayari mazungumzo kwa baadhi ya wachezaji hao yameanza na yanaendelea vizuri nba kama yatatimia basi wachezaji wapya wasiopungua watatu watatua Msimbazi mapema mwezi ujao kuongeza nguvu.


WASIKIE WADAU

Nyota wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe anaamini maboresho hayo yanaweza kuwa na matokeo chanya kwenye kikosi hicho ambacho mwakani kitaanza kucheza michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Mgunda amefanya kazi nzuri na kubwa, ni jambo jema viongozi kuamua kuendelea kuwa naye wakati wakifanya maboresho ya benchi lao la ufundi ili mchango wake uendelee kutumika kwenye timu, kiukweli umeheshimisha wazawa kwa kuivusha timu na kutinga makundi ya ligi ya mabingwa,” alisema

Kwa upande wake kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina, Mohammed Badru alisema kufanywa mapema kwa maboresho ya benchi la ufundi kwa Simba kutawasaidia kuwa na muda wa kutosha kujiandaa kabla ya michezo ya hatua ya makundi maana makocha wengi huja na falsafa zao.

“Kama mdau na mpenda maendeleo ya soka la Tanzania niwashauri Simba kuwa makini sana na maboresho yao kwa sababu hakuna eneo muhimu kwenye timu kama benchi la ufundi, wakipatia hapo basi matokeo yake yataonekana uwanjani, lakini nimpongeze Mgunda kwa kazi nzuri,” alisema.