Simba matumaini kibao kwa Pablo

Friday November 26 2021
Simbaa PIC

Kocha mkuu wa Simba SC, Pablo Franco. Picha| Simba

By Ramadhan Elias

MTENDAJI mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ameweka wazi kuwa wana matumaini makubwa na kocha mpya wa timu hiyo Pablo Franco kuelekea mechi ya Jumapili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Red Arrows kutoka Zambia.

Akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao kikosi cha Simba kinaendela na mazoezi jioni ya leo, Barbara amesema;

“Kila akija mwalimu au kiongozi mpya kwenye timu mambo yanabadilika hivyo ujio wa Pablo umebadili vitu vingi ikiwemo morali na uwezo wa wachezaji kuongezeka.

Mwalimu Pablo alianza vizuri dhidi ya Ruvu Shooting, na hii dhidi ya Arrows itakuwa mechi yake ya kwanza Dar es Salaam hivyo ni siku ya kumuangalia vyema mbinu zake,”  alisema Barbara na kuongeza;

“Tunamuamini na kwa kushirikiana na benchi zima la ufundi tunaamini atatupa ushindi katika mechi hiyo na malengo yetu kwa msimu huu ni kufika nusu fainali ya mashindano hayo” alisema Barbara.

“Hapo mwanzo kwenye Ligi ya Mabingwa tuliteleza lakini tumebaki huku na tumepanga kushinda mechi zote mbili nyumbani na ugenini katika hatua hii ili tusonge mbele kibabe” alisema Barbara.

Advertisement

Babra pia amewataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani siku ya mechi kuwapa sapoti wachezaji na timu kwa ujumla.

“Licha ya kupewa idadi ndogo ya mashabiki wanaotakiwa kuingia lakini tunawaomba mashabiki zetu wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu yao Jumapili kwani tutakuwa tukiwakilisha nchi Kimataifa,” alisema.

Simba ilitolewa katika hatua ya mwanzo ya Ligi ya  Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana na kuangukia kwenye kombe la Shirikisho ambapo Jumapili hii itatupa karata ya kwanza katika michuano hiyo dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia Saa 10:00 jioni.

Advertisement