Simba kumpigania Chikwende Ligi ya Mabingwa Afrika

MASHABIKI wa Simba wana kila sababu ya kuanza kufurahi, kwani mipango inayofanywa na mabosi wao katika kuhakikisha wanafanya vema katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa sio ya kitoto, ikiwamo kukamilisha taratibu zote za vibali vya nyota wao wapya, Perfect Chikwende na Junior Lokosa, huku wakijiandaa kumtangaza Kocha Mkuu mpya.

Tuanze na ishu ya vibali vya kina Chikwende. Mabosi wa Simba wamesema kila kitu kimekamilika kwa wachezaji hao wa kigeni waliosajiliwa dirisha dogo, ambao mmoja atatumika Ligi ya ndani na mwingine kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imekamilisha usajili wa Chikwende na vibali vyake kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na michuano mingine ya ndani kuchukua nafasi ya Mkenya, Francis Kahata atakeyecheza Ligi ya Mabingwa kama ilivyo kwa Lokosa, Mnigeria aliyesajiliwa sambamba na winga Mzimbabwe.

Lokosa anatarajiwa kutambulishwa muda wowote kuanzia leo kwa usajili wa Ligi ya Mabingwa ambao dirisha lake litafungwa Januari 30, huku mashindano ya ndani kama ligi na kombe la shirikisho (ASFC), atakuwa akiyatazama tu.

Tayari mabosi walishawaomboea vibali vyao uhamiaji na idara nyingine ili kuweza kufanya kazi bila tatizo na kwa mujibu wa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alisema muda wowote vibali vyao vitatoka ili waanze kazi.

“Kila kitu juu ya wachezaji hao kimekamilika, tunadhani watawahi kambi ya timu inayoanza Jumatatu kwa michuano ya Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, kuna jitahada zinafanywa kuona kwa kuomba ndani ya CAF, ili Chikwende aweze kutumika pia CAF,” alisema kigogo huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina.

Naye Mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori alihojiwa jana alisema kanuni mama ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zinasema mchezaji mmoja aruhusiwi kucheza au kuhama zaidi ya timu mbili katika msimu mmoja na wampigania Chikwende.

“Kutokana na kanuni hiyo tunaweza kumtumia Chikwende kwani amehama klabu moja tu FC Platinum kuja Simba, tutachofanya ni kumuombea kibali cha kucheza CAF, kama watatupatia sawa lakini ikishindikana watatueleza kwa sababu gani hivyo tusubiri huko mbele tuone,” alisema Magori.