Simba kuanza na Al Hilal, kumaliza na Mazembe

Katika kujiandaa na hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itaanza kujipima kwenye mashindano maalum wayiyoyapa jina la Simba Super Cup yatayoanza Januari 27-31.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema katika mashindano hayo kutakuwa na timu tatu Simba wenyeji na wageni wawili ambao watakuwa mabingwa wa DR Congo, TP Mazembe pamoja na Al Hilal ya Sudan.

"Mashindano haya ni kwa ajili ya timu yetu kujiandaa na Ligi ya mabingwa Afrika na kupata ushindani kutoka katika timu ambazo zenye wachezaji wakubwa kama ambao tutakwenda kukutana nao," amesema Gonzalez

"Kuhusu kocha mkuu tayari mchakato umekamilika na kuanzia  Jumamosi tutaanza kumtangaza mmoja wa wasaidizi wake ambao utafanya kazi kwa kushirikiana nao.

"Mpaka siku ya Jumatano mashindano yatakapoanza tutakuwa tayari benchi letu la ufundi limekamilika kwa maana ya kocha mkuu na wasaidizi wake wote watakuwepo," amesema Barabara.

Barbara amesema kuhusu kesi ya Jonas Mkude tayari imefikishwa katika kamati ya nidhamu ambao leo watakutana na kufanya kikao nae kisha kutoa maamuzi ambayo yatapelekwa kwa uongozi na kuamua lipi la kulichukua na kuliacha.

Ofisa habari wa Simba, Haji Manara amesema mashindano hayo wamewaalika mabingwa kwa ajili ya kuwaandaa wachezaji wao waliokuwa katika mapumziko.

"Siku ya kwanza ya mashindano tutakuwa na kocha wetu mkuu pamoja na benchi la ufundi ambao litakuwa limeanza kazi yake siku chache nyuma," amesema Manara na kuongezea viingilio vya michezo hiyo itakuwa Sh 3000 kwa mzunguko.

RATIBA KAMILI

Januari 27- Simba vs Al Hilal

Januari 29- TP Mazembe - Al Hilal

Januari 30- Simba - TP Mazembe