Simba iliwamaliza Watswana hapa tu!

Muktasari:

SIMBA imeanza kwa kishindo Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushinda ugenini 2-0 nchini Botswana juzi dhidi ya wababe wa nchi hiyo, Jwaneng Galaxy.

SIMBA imeanza kwa kishindo Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kushinda ugenini 2-0 nchini Botswana juzi dhidi ya wababe wa nchi hiyo, Jwaneng Galaxy.

Wakati mamilioni ya watazamaji wa mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana kuanzia saa 9:00 jioni za huko na saa 10:00 za Tanzania yakisubiri kuona nini kitatokea, Simba iliwashangaza wote kwa kumaliza mechi mapema.

Naam! Ni katika dakika sita tu za mwanzo wa mchezo huo Simba ilikuwa imefunga mabao mawili ya chapchap yaliyowafanya Galaxy wapoteane na kuanza kucheza kwa presha ya juu jambo lililowafanya wasipate bao na dakika 90 kumalizika kwa matokeo ya 0-2.

Mabao ya Simba yote yalitokana na mipira ya kona. Bao la kwanza alifunga kiungo wa kati Taddeo Lwanga baada ya kona iliyopigwa na Rally Bwalya kutua kwenye boksi la 18 la Galaxy na mabeki kushindwa kuuondosha ndipo Lwanga akafunga kwa shuti la wastani.

Hata bao la pili ni vivyo hivyo, kwani Benard Morrison alianza kona fupi kwa Bwalya aliyepiga krosi kwenye boksi la Galaxy ambao walijichanganya tena na beki wao kumtengea mpira kwa kichwa John Bocco aliyeokota dodo akifunga kwa shuti kali.

Mabao hayo yaliwapa wakati mgumu Galaxy. Sio kwamba uwezo wao ni mdogo, lakini waliingiwa na hofu ya kufungwa mabao mengi zaidi na kupoteza asili ya mchezo waliouzowea.

Kadri muda ulivyozidi kwenda Simba iliendelea kulisakama lango la Galaxy kwa kushtukiza huku umakini mkubwa ukiwekwa katika nyakati za kujilinda.


UKUTA IMARA

Moja ya karata ambazo benchi la ufundi la Simba lilicheza vizuri juzi chini ya kocha Thierry Hitimana, ni kumuanzisha beki mkongomani Henoc Inonga ‘Varane’ sambamba na Pascal Wawa kwenye ukuta.

Varane alikuwa kwenye kiwango bora cha manufaa kwa Simba, kwani kuanzia dakika ya 35 ya mchezo Galaxy walilisakama lango la Simba mara kwa mara, lakini uobra wa beki huyo ulikuwa kizuizi kwao.

Kuna wakati beki huyo aliokoa kwa vichwa mara nne mfululizo na muda mwingine kwa miguu na wakati mwingine alituliza presha kwa kupiga pasi za mbali kama ambavyo hufanya Wawa.

Nje ya uwezo wa mabeki, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Shomary Kapombe na Wawa, lango la Simba pia lilikuwa salama kutokana na ubora wa kipa Aishi Manula ambaye alikuwa na mchezo mzuri wa kuwazuia Galaxy kupata bao hata moja nyumbani kwao.


MORRISON, DILUNGA WALISAPRAIZI

Mara nyingi Simba imekuwa ikitumia viungo wengi na mshambuliaji mmoja kwenye mechi zake, lakini juzi benchi la ufundi la Simba liliwasapraizi Galaxy.

Lilianza na mawinga wawili wenye spidi na nguvu - Benard Morrison na Hassan Dilunga ambao waliipa tabu Galaxy wakati ikiwa na mpira na bila mpira.

Wawili hao walikuwa wakishambulia na kukaba na pale Galaxy walipotaka kufunguka na kutafuta bao walijikuta wakishindwa kwani namba ya wakabaji kwa Simba iliongezeka kutokana na uwepo wa Dilunga na Morrison kwenye eneo la chini.


NINI WAFANYE

MARUDIANO

Licha ya kwamba Simba ilishinda mechi hiyo ugenini, lakini si kigezo cha kuwabeza Galaxy na kuingia kinyonge kwenye mechi ya marudiano Oktoba 22 itakayopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.

Simba inatakiwa kufanyia marekebisho mbinu zake na kuongeza umakini katika kutengeneza nafasi kwani tangu kuondoka kwa viungo Clatous Chama na Luis Miquissone a haijafunga bao la ‘muvu’ linaloonekana kuwa limetengenezwa na timu.

Katika mechi tano kubwa walizocheza msimu huu ukianzia Simba Day waliyolala 1-0 kutoka kwa TP Mazembe, mechi ya Ngao ya Jamii waliyofungwa 1-0 dhidi ya Yanga, ile ya kwanza ya Ligi Kuu Bara waliyotoka suluhu na Biashara, mechi ya pili ya Ligi Kuu waliyoshinda 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na ile ya juzi, Simba imefunga mabao matatu tu. Kati ya hayo mabao mawili ni ya juzi dhidi ya Jwaneng yaliyotokana na mipira iliyokufa na moja dhidi ya Dodoma Jiji lilitokana na akili kubwa binafsi ya kipa Manula ambaye alipiga mpira mrefu wa juu uliopigwa kichwa kimoja tu na Chris Mugalu, aliyemtengea mfungaji wa bao hilo, Meddie Kagere.

Simba inapaswa kuwasahau Chama na Luis ambao katika Ligi Kuu msimu uliopita walihusika moja kwa moja katika mabao 42 kati ya mabao 78 yaliyofungwa na timu hiyo na kutwaa taji la nne mfululizo la ligi.

Inapaswa kujiimarisha haraka katika kutengeneza nafasi nyingi za mabao ili kuendeleza ubabe wake wa Afrika ambako imefunika kwa kufika robo fainali mara mbili katika misimu mitatu iliyopita.

Katika mechi ya marudiano inahitaji kujilinda kwa nidhamu ili kulinda ushindi wa mabao mawili ugenini, licha ya kwamba Galaxy inahitaji kushinda bao 3-0 ili isonge mbele. Simba haipaswi kuruhusu bao la mapema kwani linaweza kuwatoa mchezoni na kuwaruhusu Galaxy kuwapa wakati mgumu.

Endapo Simba itaongezea hayo kwenye mipango yake, basi itafuzu hatua ya makundi na kuendelea kuwakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa.


WENYEWE WANASEMAJE?

Kocha mkuu wa timu hiyo, Didier Gomes baada ya mchezo wa juzi kumalizika alieleza kuwa pamoja na ushindi, bado kazi haijaisha na wanajipanga kushinda nyumbani ili kuhitimisha jukumu zito walilonalo.

“Mpira huwa matokeo yake hayatabiriki. Tunashukuru kwa ushindi lakini hautupi kiburi cha kusema kuwa tumefuzu hatua ya makundi tayari,” alisema Gomes.

“Pia Jwaneng sio timu nyepesi. Wachezaji wao wote wana uwezo mkubwa na wanaipambania timu, hivyo hatupaswi kuwabeza bali kujipanga kupambana nao na kushinda nyumbani ili kusonga mbele kwani uwezo huo tunao.”

Naye kocha Mkuu wa Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli alisema kuwa licha ya kupoteza mchezo huo lakini wamejipanga kuja Tanzania kupambana.

“Mwamuzi alitunyima penalti mbili kwenye mechi ya leo (juzi) ambazo kama tungezipata matokeo yangekuwa sawa, lakini ndiyo tayari mchezo umeisha,” alisema kocha huyo.

“Sasa tunarudi kujipanga kwenye mchezo ujao kwani tunajua Simba ni timu hatari zaidi ikiwa nyumbani.”

Mchezaji wa zamani wa Yanga na na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema kuwa Simba inapaswa kujipanga zaidi kwenye mechi ya marudiano kwani mpira unadunda, hivyo unaweza kusababisha matokeo yasiyotarajiwa.

“Matokeo waliyoyapata kule hayawathibitishii kuwa wamefuzu hatua ya makundi, hivyo wanahitaji kuingia kwa tahadhari kwenye mchezo wa marudiano ili kushinda au kutoka sare, ndipo wasonge mbele kwani matokeo ya soka huwa hayatabiriki,” alisema.