Simba: Hatuachi mtu Botswana

‘TULIENI tu! Hatuachi mtu.’ Ndio mzuka mpya wa Kocha wa Simba, Didier Gomes atakapokwenda na kikosi chake kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa huko Botswana.

Gomes kwa sasa ana siku 10 tu za kuimarisha safu yake ya ushambuliaji na staili ya kiuchezaji ili kuhakikisha hawawaachi salama Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo.

Hata hivyo, safu hiyo ya ushambuliaji ya Simba ndio idara pekee inayoipasua kichwa timu hiyo kutokana na mwanzo mbaya katika mechi za hivi karibuni hasa zile za mashindano

Katika mechi nne moja ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe, moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga pamoja na mbili za Ligi Kuu ilizocheza na Biashara United na Dodoma Jiji, Sim ba imefunga bao moja tu huku ikitoka patupu katika mechi tatu.

Mbinu ya kushambulia kwa kasi inaweza kuwa na faida kubwa kwa Simba dhidi ya Jwaneng kutokana na udhaifu wa timu hiyo ya Botswana katika safu yake ya ulinzi pindi inapokutana na washambuliaji wenye kasi.

Timu hiyo imekuwa ikicheza soka la taratibu la pasi fupifupi kuanzia nyuma na mara kwa mara imeonekana kutohimili kukabiliana na washambuliaji wenye kasi.

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema; “Ni wakati wa benchi la ufundi pamoja na uongozi, kuanza kuwajua kiundani wapinzani wao kwa maana wanacheza soka la aina gani, kisha waanze kuwaandaa wachezaji kutokana na uhalisia wa kile watakachokwenda kukutana nacho, wachezaji nao wajitoe kikamilifu.”

Pia, walinzi wa Jwaneng Galaxy hasa wale wa kati wamekuwa wakifanya makosa binafsi ambayo yamekuwa yakitumiwa vizuri na washambuliaji wa timu pinzani.

Mtindo wa kukaba kwa nafasi (zonal marking) umekuwa ukiiathiri timu hiyo kwa kuwapa uhuru wa kufanya maamuzi washambuliaji wa timu pinzani pale wanapokuwa jirani na lango lao tofauti na iwapo wangekuwa wanazuia kwa kukaba mtu (man marking)

Uthibitisho wa hilo, katika mechi tano za mashindano zilizopita za timu hiyo ya Botswana, imepoteza mechi nne, ikishinda moja, imefunga mabao matatu tu huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Hata hivyo, pamoja na rekodi hiyo isiyo ya kuvutia ya safu ya ulinzi ya Jwaneng Galaxy pamoja na historia nzuri ya Simba katika awamu zilizopita, kocha msaidizi wa Kagera Sugar, George Kavila alisema Simba inapaswa kuwa na tahadhari kubwa.

“Mechi za ugenini zina namna yake ya kucheza, jambo kubwa wawaheshimu wapinzani, wasijiamini sana kutokana na mafanikio yaliyopita, kwa kuwa kuna wachezaji muhimu na wazuri waliondoka na waliwaleta wengine ambao bado hawajazoeana.”

Uwepo wa mshambuliaji Bernard Morrison kikosini unaweza kwa kiasi kikubwa kuwa msaada kwa Simba kutokana na kasi na ubunifu wa nyota huyo pindi anapokuwa na mpira jirani na lango la timu pinzani pamoja na maamuzi yake ya haraka katika kufunga ama kupiga pasi ya mwisho.

Licha ya winga Pape Sakho kuwa na nafasi finyu ya kucheza huku Peter Banda akiwa bado hajamudu vyema mfumo wa Simba, Gomes anaweza kuwatumia Kibu Denis, Yusuph Mhilu na Duncan Nyoni ambao kasi, uwezo wao wa kuwalazimisha walinzi wa timu pinzani kufanya makosa pamoja na uharaka wao wa kufanya uamuzi unaweza kuwa mwiba kwa Jwaneng Galaxy.

Akizungumzia hilo, Pawasa alisema “Hatuwezi kukwepa ukweli wa Clatous Chama na Luis Miquissone walikuwa muhimu Simba, ila kwa sasa tunapaswa kuangalia nini kinapaswa kufanyike kwa kuwatumia mastaa walionao.”

Straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ally Pazi Samatta alisema “Mafanikio ya miaka minne nyuma, wachezaji wanajiona wanacheza sana, wanafunga sana, sasa hilo waondoe kichwani mwao, washambuliaji ni kazi yao kufunga waongeze umakini, wajitolee kwa ajili ya timu yao, ndipo wataanza kwa kishindo dhidi ya Botswana Jwaneng Galaxy,”