Simba, Fountain hapatoshi kwa Mkapa

Wednesday June 22 2022
fountain pic
By Oliver Albert

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika mechi maalumu itakayowakutanisha Simba Queens dhidi ya Fountain Gate PrincessvJumamosi kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa ni wa kuadhimisha miaka 25 ya Taasisi ya Fursa Sawa kwa Wote( EOTF) inayoongozwa na mke wa Rais wa awamu ya tatu , Anna Mkapa.

Raisi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema wameamua kumuunga mkono mama Mkapa kwa sababu ameona soka ni mchezo wa jamii na taasisi yake inahudumia jamii.

"Tulipanga icheze Yanga Princess na Simba Queens, lakini Yanga wana udhuru na unajua ligi ya wanawake imemalizika hivyo wachezaji wao wametawanyika.

"Simba imekuwa rahisi kwa sababu bado wako kambini wanajiandaa na mashindano ya kimataifa ya kanda ya Cecafa kutafuta nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Fountain Gate Princess ni rahisi kuwapata kwani wengi wako shule pale pale, " amesema Karia.

Karia amesema katika kumuunga mkono mama Mkapa watapeleka sehemu ya mapato ya mchezo wa Ngao ya Jamii msimu ujao katika mfuko wa Taasisi ya Fursa Sawa kwa Wote.

Advertisement

Naye mwenyekiti wa taasisi hiyo, Anna Mkapa amesema wamechagua mechi ya timu za kinamama ili wamama wengi waone michezo ni ajira.

Amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1997 wakati mumewe akiwa ni rais na ina malengo matatu ikiwemo kuwasaidia kinamama na vijana kujitegemea kiuchumi, kuwasaidia kinamama na watoto katika masuala ya afya na kusaidia watoto wa mitaani.

Naye Ofisa Habari wa TFF Clifford Ndimbo amesema mchezo huo ambao hakutakuwa na kiingilio utaanza saa 9:30 na mgeni rasmi atakuwa ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

" Kabla ya mchezo wa wanawake kutakuwa na mechi ya utangulizi kati ya wake wa viongozi dhidi ya wajasiriamali, hivyo tunawaomba mashabiki wa soka kufika kwa wingi, " amesema Ndimbo.

Advertisement