Simba, Al Hilal hakuna mbabe

MABINGWA wa Sudan Klabu ya Al Hilal wamelazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba katika mchezo mkali wa kirafiki wa Kimataifa uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Al Hilal ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa nyota wake, Makabi Lilepo dakika ya sita tu ya mchezo huku Habib Kyombo akaiandikia Simba bao la kusawazisha dakika ya 81 kipindi cha pili.

Al Hilal iliwasili nchini Jumatatu ya Januari 25 kwa mwaliko maalumu wa Simba ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kimkataba baina ya timu hizo zinazojiandaa na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Mchezo wake wa kwanza tangu ilipowasili ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC Januari 26, katika mechi iliyokuwa kali na ya kusisimua iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Baada ya hapo Al Hilal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wake wa pili wa kirafiki uliochezwa Januari 31 Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam.

Miamba hii ya Sudan inakumbukwa zaidi na Watanzania kwani ndio timu iliyoiondosha Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuifunga jumla ya mabao 2-1 kwenye hatua ya pili ya mtoano.

Baada ya mchezo huu Simba itasafiri hadi nchini Guinea kuanza safari yake ya matumaini katika hatua za makundi za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Horoya, mechi itakayochezwa Februari 11.

Kwa upande wa Al Hilal nao wanakabiliwa na kibarua kizito Februari 11 wakati watakapoanza pia safari ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Simba iko kundi C sawa na timu za Raja Casablanca (Morocco), Horoya (Guinea) na Vipers ya Uganda huku Al Hilal iko kundi B na Al Ahly (Misri), Mamelodi Sundown (Afrika Kusini) na Coton Sport ya Cameroon.