Shoo ya Marumo inafia hapa...
RAMANI kamili imechorwa na Yanga kuhakikisha wapinzani wao katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Marumo Gallants ya Afrika Kusini wanakutana na kitu kizito watakapotua Kwa Mkapa katika mechi yao ya mkondo wa kwanza Jumatano hii.
Picha kamili liko hivi: Yanga imewasoma wapinzani wao hao ambao wako katika hatari ya kushuka daraja kule kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini lakini wanatisha kwenye Kombe la Shirikisho.
Lengo la kuwachimba Gallants ni kujua mambo yapi yanawapa mafanikio Afrika na kipi kinawakwamisha kule kwenye ligi ya PSL na siri zao zimenaswa.
WANAFUNGIKA
Marumo licha ya kumaliza vinara wa kundi A lililokuwa pia na timu za USM Alger ya Algeria, Saint-Eloi Lupopo ya DR Congo na Al Akhdar ya Libya, wakiwa na pointi 12 baada ya mechi 6, ni timu ambayo inafungika na inaruhusu mabao mengi kwani ilimaliza ikiwa imefunga mabao 12 na kufungwa mabao 10.
Ilifungwa mabao 4-1 na Al Akhdar kule Libya na ikapasuka 2-0 ugenini dhidi ya USM Alger, lakini ikaja kulipa kisasi kwa kushinda 4-1 dhidi ya Al Akhdar na kushinda pia 2-0 dhidi ya USM Alger -- hii ni taa nyekundu kwa Yanga kwamba hata ikishinda kwa mabao manne Kwa Mkapa isije kushangilia sana na kudhani kuwa mechi imeisha kwa sababu Gallants wana uwezo wa kukufunga kwao kama ulivyowafunga kwako.
Timu hiyo ambayo kwenye Ligi ya PSL inashika nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 29 baada ya mechi 28, imefungwa mabao 30 huku yenyewe ikifunga mabao 27 tu, lakini ni timu inayocheza kwa staili ya piga nikupige kwani katika moja ya mechi zake za makundi ya Shirikisho msimu huu ilishinda 3-2 dhidi ya Lupopo.
Jambo la kuchunga ni kwamba Marumo ni wakali sana kwenye uwanja wa nyumbani, wameshinda mechi zote nne hadi kufikia sasa kwa jumla ya mabao 10-3, hawajapoteza mchezo wala kutoa sare katika Kombe la Shirikisho msimu huu.
Yanga ambayo ilimaliza kinara wa Kundi D ikiwa na pointi 13, moja tu zaidi ya Marumo, ilifunga mabao tisa na kuruhusu manne, ikiwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi msimu huu (manne) sawa na Asec Mimosas ambayo pia iko nusu fainali na US Monastir, ambayo ilikwamia kwenye robo fainali.
YANGA ITEMBEE NA HAWA
Marumo inacheza kitimu, lakini ina watu muhimu zaidi ambao wanaifanya ilete shida kwa wapinzani na mmoja wao ni straika wao, Ranga Chivaviro, ambaye amekuwa kwenye kiwango bora katika michuano hii kwani ndiye kinara wa mabao wa Shirikisho msimu huu, akilingana na Fiston Mayele wa Yanga, kila mmoja akiwa na mabao matano.
Wakati kina Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca, wakiandaliwa kumdhibiti, wapo watu wengine ambao ni hatari katika kumtengenezea nafasi na pia kuasisti, kama ambaye msimu huu ametengeneza nafasi 15, ametoa asisti mbili na kufunga bao moja na yupo piaLesiba Nku ambaye amechangia mabao matatu akifunga mawili na kutoa asisti moja.
KIPA LA MIPASI
Licha ya kushika nafasi ya tatu kati ya timu zilizoruhusu mabao mengi zaidi kati ya timu 16 zilizoshiriki hatua ya makundi ya Shirikisho msimu huu (nyuma ya ASKO Kara ya Togo iliyoruhusu mabao 15 na Al Akhdar iliyofungwa mabao 12), kipa wa Marumo, Washington Arubi ni mtu wa kuchunga sana katika kuanzisha mashambulizi ya timu hiyo.
Kipa Arubi anashika nafasi ya pili tu nyuma ya Djigui Diarra wa Yanga katika chati ya vinara wa kupiga pasi miongoni mwa makipa wa timu nne za nusu fainali.
Arubi amepiga pasi 108 huku pasi 35 kati ya hizo amewapasia wachezaji wake walio katika nusu ya mpinzani, yaani anapiga mpira unaovuka mstari wa katikati na kumfikia kimafanikio mchezaji wa timu yake.
Katika hilo, anazidiwa na Diarra tu, ambaye hadi sasa katika michuano hii amepiga pasi 186 zilizowafika walengwa, huku pasi 68 kati ya hizo akiwapa wachezaji wa Yanga walio katika eneo la mpinzani, yaani anapiga mpira unavuka mstari wa katikati ya uwanja na kuanzisha mashambulizi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo za Caf, kipa huyo wa Marumo pia anaongoza kwa kuokoa (saves) nyingi (20) kati ya makipa wa nusu fainali, akifuatiwa na Oussama Benbot wa USM Alger (saves 18), kisha Diarra (saves 13) na Charles Ayayi wa Asec aliokoa hatari 8.
CHIVAVIRO AVIMBA
Kinara wa mabao wa Marumo, Chivaviro ametamba kuwa kazi yake ni kufunga na anakuja Tanzania kwa kazi hiyo huku akitambia uzoefu wa kocha wake Dylan Kerr na soka la Bongo umemuongezea morali.
Akizungumza na Mwanaspoti, straika huyo alisema ana vita mbili dhidi ya Yanga ikiwa ni pamoja na kuipambania timu yake kutinga fainali na kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo dhidi ya Mayele.
"Nawaheshimu Yanga, natambua ni timu bora na ndio maana imefika hatua hii ya mashindano na sisi ni bora, tunakuja Tanzania kutafuta rekodi ya kupata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wetu nikiwa kama mshambuliaji sina ninayemuhofia nakuja kufanya majukumu yangu;
"Mayele ananipasua kichwa kutokana na idadi ya mabao yangu na yake kuwa sawa mechi mbili kati yetu ndio zitaamua nani atakuwa mfumania nyavu bora, nakitaka kiatu, nakuja Dar es Salaam kukamilisha majukumu yangu kwa kutumia kila nafasi nitakayoipata."
Chivaviro alisema wao kama wachezaji wanahitaji matokeo mazuri ugenini ili kwenda kukamilisha kazi nyumbani kwao na hatimaye kutinga hatua ya fainali huku akisisitiza kuwa wanajuvunia kunolewa na kocha ambaye ni mzoefu wa ligi ya Tanzania.
"Kerr kocha wetu mkuu amepata nafasi ya kufundisha soka la Tanzania na amefundisha timu kubwa ya Simba hivyo anafahamu soka la nchi hiyo, amekaa na sisi kutupa mbinu ili tuweze kufanya vizuri, hilo linatuma nafasi nzuri ya kukaa sawa kisaikolojia," alisema Chivaviro ambaye kwenye Ligi Kuu ya Afrika Kusini ametupia wavuni mabao tisa akicheza mechi 17.
NABI HUYU HAPA
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amewataka wachezaji wake kuachana na shangwe la kufuzu nusu fainali na kuukaribia ubingwa wa Ligi Kuu na badala yake kujiandaa kiakili kucheza mechi kubwa katika historia yao dhidi ya Marumo.
"Tunajua makosa yao wanavyocheza ugenini kuna mechi wamekuwa wakikutana na wakati mgumu wa kupoteza lakini wanakuwa wakali zaidi wanapokuwa nyumbani, tumeangalia ni mbinu gani za kutumia lakini pia tutawapa kila kitu wachezaji wetu kupitia darasa letu maalum la mikanda ya wapinzani."
Aidha, Nabi ametoa maagizo ya kiitelijensia kwa mabosi wake akitaka kuongezwa ulinzi kambini kwao akitaka watu kutofuatilia mazoezi yao wakiwemo mashabiki wa timu yake.
REKODI YA KERR
Kocha wa Marumo, Dylan Kerr, aliwahi kuifundisha Simba lakini hakuwahi kuifunga Yanga wala kupata japo bao moja msimu wa 2015/2016.
Katika msimu huo Simba ilimaliza nafasi ya tatu kwa pointi 62 nyuma ya Azam (64) huku Yanga ikitwaa ubingwa kwa pointi 73. Chini ya Kerr, Simba alipoteza mechi zote mbili kwa jumla ya mabao manne ambapo mchezo wa kwanza uliopigwa Septemba 26 mwaka 2015 alifungwa 2-0 na kupoteza tena 2-0, Februari 20, 2016.
MATOKEO YA SHIRIKISHO YANGA
US Monastir 2-0 Yanga
Yanga 3-1 TP Mazembe
Real Bamako 1-1 Yanga
Yanga 2-0 Real Bamako
Yanga 2-0 US Monastir
TP Mazembe 0-1 Yanga
ROBO FAINALI
Rivers 0-2 Yanga
Yanga 0-0 Rivers
MARUMO GALLANTS
Marumo 4-1 Al Akhdar
Lupopo 1-2 Marumo
USM Alger 2-0 Marumo
Marumo 2-0 USM Alger
Al Alkhdar 4-1 Marumo
Marumo 3-2 Lupopo
ROBO FAINALI
Pyramids 1-1 Marumo
Marumo 1-0 Pyramids
NUSU FAINALI
Yanga ?-? Marumo