Shikhalo afichua siri penalti ya Onyango
KIPA wa Yanga, Mkenya Faruk Shikhalo ameeleza vile alivyomtania rafiki yake Joash Onyango baada ya kupangua penati ya beki huyo wa Simba kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.
Yanga iliibuka na ushindi wa penati 4-3 baada ya dakika 90 za mchezo huo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Aman kumalizika suluhu.
Shikhalo ambaye ni rafiki wa Onyango amefichua kuwa alimcheka na kumtania kwa kusema, "Ulitaka kunikosesha pesa kama ilivyokuwa mechi iliyopita ya watani wa jadi ambayo imalizika kwa sare ya bao 1-1."
Kipa huyo bora wa Mapinduzi, amesema Onyango aliishia kucheka na maisha ya kawaida yakaendelea baina yao maana ni kama ndugu kutokana na ukaribu uliopo baina yao licha ya kuwa klabu wanazozichezea ni mahasimu.
Mchezo ambao Shikhalo amemaanisha kuwa Onyango aliwakosesha pesa ni ule wa Novemba mwaka jana ambapo walikuwa wakiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa Michael Sarpong lakini kuchomoa kwa beki huyo kuliwafanya Yanga kushindwa kujikusanyia donge nono.
Wachezaji wa Yanga waliahidiwa mamilioni ya pesa kama wangeifunga Simba ndio maana Shikhalo alimtania Onyango kuwa alitaka kuwakosesha mamilioni mengine ya Kombe la Mapinduzi viusiwani Zanzibar.
Shikhalo tulikuwa naye leo, Jumamosi ya Januari 16, 2021 kwenye Ofisi zetu za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited na kuzungumza mambo kibao ikiwemo kile kitu ambacho kimezua gumzo mitandaoni.
Alionekana kumtuma mmoja wa watumishi wa Yanga akakichukue golini hivi unajua ilikua nini? basi usikose kufuatilia mahojiano yetu na kipa huyo wa Kimataifa wa Kenya ndani ya gazeti la Mwanaspoti pekee.