Sheva atua Geita Gold, ajifunga miwili

Thursday August 04 2022
New Content Item (1)
By Damian Masyenene

Mwanza. HUKO Geita kunazidi kunoga baada ya timu kuendelea kuanika vifaa vyake vipya ilivyonasa kwenye dirisha kubwa la usajili kuelekea msimu mpya wa mashindano ikiwemo michuano ya kimataifa.

Baada ya jana kushusha kitasa kutoka Ghana, Shown Oduro, leo klabu hiyo imemtambulisha Miraji Athuman 'Sheva'.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ametambulishwa klabuni hapo ikiwa ni jitihada za kuboresha eneo la ushambuliaji linaloongozwa na George Mpole na Dany Lyanga.

Sheva ametua kwa wachimba Dhahabu hao kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kumalizana na KMC ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hatua ya kumnasa Sheva ni kama matajiri hao wa Dhahabu wamepindua meza kibabe baada ya nyota huyo kutajwa kutua Ihefu ya jijini Mbeya ambayo imepanda daraja msimu huu.

Nyota huyo ameliambia Mwanaspoti kuwa ni furaha kwake kujiunga na timu hiyo na amejipanga kupambana kuhakikisha anaisaidia timu hiyo kufikia malengo yake katika michuano ya ndani na kimataifa.

Advertisement

Miraji anakuwa mchezaji wa tano kutangazwa kusajiliwa na Geita Gold katika dirisha hili, wengine waliomalizana na timu hiyo ni George Wawa (Dodoma Jiji), Hussein Kazi (Polisi Tanzania), Arakaza MacAthur (Power Dynamos) na Shown Oduro (Ghana).

Advertisement