Senegal yafunga hesabu kibabe ikinusa Kombe la Dunia

Wednesday October 13 2021
senegal pic
By Charles Abel

Senegal imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya mtoano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kwa mwakani kwa upande wa bara la Afrika baada ya leo kujihakikishia uongozi wa kundi H.

Ushindi wa mabao 3-1 ambao 'Simba Wa Teranga' wameupata ugenini dhidi ya Namibia umewafanya wafikishe jumla ya pointi 12 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu yoyote katika kundi hilo.

Congo inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili na Togo yenye pointi moja ambazo muda mfupi ujao zitakutana, hakuna itakayoweza kuifikia Senegal hata ikishinda mechi zote tatu kwani Congo inaweza kumaliza ikiwa na pointi 11 na Togo hata ikishinda mechi tatu zilizobaki ikiwemo ya leo itamaliza ikiwa na pointi 10 tu.

Namibia iliyopo nafasi ya pili na pointi zake nne, hata ikipata ushindi katika mechi zake mbili zilizobakia katika kundi hilo dhidi ya Congo na Togo, itamaliza ikiwa na pointi 10 tu.

Shujaa aliyeihakikishia Senegal tiketi ya kucheza hatua ya mwisho ya mtoano kusaka nafasi tano za kuiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia mwakani alikuwa ni nyota wa nchi hiyo anayeitumikia Alanyaspor ya Uturuki, Famara Diedhiou aliyepachika mabao yote matatu 'Hat trick' katika mechi hiyo.

Diedhiou alianza kuifungia Senegal bao la kuongoza katika dakika ya 22 lakini dakika tano baadaye Peter Shalulile akaisawazishia Namibia katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Independence jijini Windhoek.

Advertisement

Dakika sita tu baada ya mapumziko, Diedhiou aliipatia Senegal bao la pili na katika dakika ya 84 akahitimisha kalamu ya mabao kwa kuifungia timu yake bao la tatu.

Kwa kufuzu huko, Senegal sasa inasubiria timu nyingine tisa ambazo zitapangiwa droo ya kucheza mechi za mtoano kusaka nchi tano zitakazofuzu Kombe la Dunia kwa upande wa Afrika

Advertisement