Selengo: Simba inachukua tena

Tuesday September 15 2020
selengo pic

MSANII wa filamu za kibongo, Ben Branco maarufu Selengo amesema licha ya Simba, kugawana pointi moja moja na Mtibwa Sugar,  anakiamini kikosi hicho kitatetea ubingwa msimu huu.

Msanii huyo ambaye hajifichi kuwa ni shabiki wa Simba lialia, amesema kinachomwaminisha chama lake litachukua ubingwa mara nne mfululizo ni kutokana wachezaji kuwa na uzoefu mkubwa, hivyo wanaweza wakapambana kwenye mechi ngumu na nyepesi.

"Achana na matokeo ya Mtibwa Sugar, kutoka nao sare ya bao 1-1, ninachokiangalia ni kikosi kina wachezaji ambao wana uwezo wa kushindana wao kwa wao kabla ya kukutana na wapinzani wao, hilo litasaidia kupata matokeo yakuisaidia timu kuchukua ubingwa mara nne mfululizo,"amesema  Branco nakuongeza kuwa.

"Mfano safu ya mbele unaona kumeongezeka wachezaji ambao akikosekana John Bocco na Meddie Kagere wanaweza wakaisaidia timu kupata matokeo kama huyo, Larry Bwalya, Benard Morrison, Luis wote hao wanaweza wakafunga,"amesema.

Amesema anatambua Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ni ngumu, lakini anaona itawapa mastaa wa Simba kuonyesha uwezo zaidi kwamba ubingwa waliochukua mara tatu mfululizo sio kwa bahati mbaya.

"Wachezaji wanapaswa kujua kwamba tunawategemea, hivyo wanatakiwa kuwadhihirishia wapinzani wao kwa kuchukua taji hilo tena, ndicho kitakachowafunga midomo kwamba sisi sio levo yao,"amesema.

Advertisement
Advertisement