SAIDO: Kishindo Kinakuja!

Muktasari:

YANGA wana kitu moyoni. Wana hasira wakiona watani wao Simba wakipaa kwa ubora sio tu ndani, bali hata Afrika. Sasa staa wao mmoja mkubwa Said Ntibazonkiza ‘Saido’ amehudhuria kikao kimoja cha mabosi na wachezaji wenzake wote kisha alipotoka akasema sasa safari ya ubingwa inaanza.

YANGA wana kitu moyoni. Wana hasira wakiona watani wao Simba wakipaa kwa ubora sio tu ndani, bali hata Afrika. Sasa staa wao mmoja mkubwa Said Ntibazonkiza ‘Saido’ amehudhuria kikao kimoja cha mabosi na wachezaji wenzake wote kisha alipotoka akasema sasa safari ya ubingwa inaanza.

Iko hivi. Juzi, Jumanne jioni vigogo wa Yanga walitua mazoezini wakiongozwa na mdhamini wao, Ghalib Mohamed, anayemiliki Kampuni ya GSM na msaidizi wake Injinia Hersi Said wakiambatana na vigogo Hussein Nyika, Said Ntimizi na Karigo Godson.

Walipomaliza mechi moja ya kirafiki dhidi ya African Lyon, jamaa walikutana hapohapo uwanjani na vijana wao na kuteta kwa dakika 36 juu ya ramani ya ubingwa wakiwa ndio vinara wa Ligi Kuu na walipomaliza tu Saido akatema cheche.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, Saido alisema kwa kikao ambacho wamefanya na jinsi alivyowaona wenzake mazoezini siku mbili pamoja na kiwango cha mchezo dhidi ya Lyon kuna mshtuko unakuja.

Staa huyo wa Burundi alisema jinsi alivyoona walivyoiva alilazimika kushtuka na kuamua kwenda kwanza ufukweni kujiweka sawa kabla ya kuungana nao akiwaona wenzake tayari gari limewaka.

“Nilipofika mliniona naangalia mechi, nimeona kwamba nalazimika kuanza mazoezi mwenyewe, watu wameiva, kila mmoja yuko sawa, hili limeniambia kwamba kwanza natakiwa kujiandaa na ndio maana nikaanzia ufukweni kwanza ili nikija uwanjani twende sawa,” alisema Saido.

“Watu wameimarika sana nilikuwa namuangalia hata ndugu yangu Fiston (Abdulrazack) sasa yuko tayari kutoa kile ambacho najua anacho, ameiva na yuko tayari tofauti na wakati anafika alihitaji muda kuzoea soka la hapa, sio tu yeye kila mmoja namuona kuna kitu anataka kufanikisha na timu inakuwa hivi.

“Sasa tuna sura ya ushindani na naamini kama Mungu akituweka salama, kama hivi, basi kuna kitu tunarejea kukipigania kwa nguvu kuliko huko nyuma, mashabiki warudi kutuunga mkono huu ni mwaka wetu.”


KIKAO CHA MABOSI

Mshambuliaji huyo alisema ramani ambayo mabosi wamewapa katika kikao hicho cha juzi ndio sababu kubwa inayomfanya kuanza kuamini kwamba wataondoka na kitu.

“Kile kikao pale pia kimetoa mwanga mkubwa sana, nimeridhika kuona viongozi nao wanataka kitu msimu huu na wako pamoja na timu.”