Saido baibai, Sarpong agoma

YANGA iko kwenye majadiliano ya kuachana na fundi wa faulo, Saido Ntibazonkiza. Lakini straika mwenye mabao manne Michael Sarpong amegoma kuachwa akitaka mkwanja mnene usiopungua Sh 71 Milioni.

Vigogo wa Yanga hawajaridhishwa na kiwango chake, lakini Sarpong amekomaa alipwe mamilioni hayo ili aachane nao, jambo linaloonekana gumu la kuwaingiza hasara.

Kutokana na dau analolitaka Sarpong, linachukua muda mwingi wa mabiosi wanaokuna kichwa wasijue la kufanya dhidi ya sharti hilo.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili wa Yanga, alilipenyezea ukweli huo Mwanaspoti na kusema jambo la Sarpong linawapasua kichwa, kutokana na kutaja dau kubwa wakati alishindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.

“Wakati Sarpong anasajiliwa alitarajiwa kufanya makubwa, lakini hakufikiwa kiwango hicho, sasa pesa aliyotaja ni kubwa ambayo inatupasua kichwa hatuelewi tufanye nini hadi sasa, kwani ni jambo lililochukua muda mrefu kuliamua,” alifichua mjumbe huyo aliyekataa kutajwa jina gazetini.

Aliongeza mbali na Sarpong, mastaa wengine wanaojadiliwa kutemwa ni kipa Faruk Shikhalo (huru) na Saido Ntibanzonkiza ambaye amebakiza miezi michache.

“Japo Shikhalo kamaliza mkataba kuna viongozi wanamhitaji na kocha ameomba apewe muda wa kumuangalia kwa ajili ya safari yake ya msimu ujao, ila kwa Saido amebakiza miezi michache na tunamjadili namna ya kuachana naye.”

Sarpong alijiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sport ya Rwanda, hivyo mkataba unaowapasua kichwa vigogo wa Yanga ni wa mwaka mmoja.


MORO AAGA

Aliyekuwa nahodha wa klabu hiyo, Lamine Moro amesema ni furaha na heshima kuvaa jezi ya timu ambayo aliyoifikiria kabla ya miaka miwili kabla ya kujiunga nao.

Moro amefunguka hayo siku chache baada ya kuvunja mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa msimu mmoja uliokuwa umesalia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram amewashukuru viongozi, wanachama na wachezaji wa timu hiyo kwa muda waliofanya kazi pamoja.

“Kwa pamoja tumepambania mazuri katika hali ngumu na rahisi tukitaka kuona timu inapata mafanikio kila siku nitaikumbuka Tanzania na Yanga nawatakia kila lakheri,” aliandika Lamine.