Rekodi zampa Failuna shaba

WANARIADHA 91 akiwamo Mtanzania, Failuna Abdi wana kibarua cha kusaka bingwa wa Olimpiki msimu huu kwenye mbio za marathoni za wanawake, ambazo kama Failuna atautumia vema uzoefu na rekodi yake kimataifa ana uhakika wa kurejea na medali ya shaba au nyingine yoyote.

Failuna atachuana Jumamosi akiwa ni Mtanzania wa kwanza kuchuana kwenye michezo ya msimu kabla ya Alphonce Simbu na Gabriel Geay kuchuana Jumapili.

Mbio zote zitaanzia kwenye eneo la Sapporo Edori Park kuanzia saa 1 Asubuhi.

Tayari timu ya Tanzania imewasili jana kwenye mji huo ikitokea Tokyo ambako ilifikia Ijumaa iliyopita na kutimiza taratibu zote za ushiriki wao kwenye mbio ya marathoni ambazo Failuna atafungua dimba kwa timu ya Tanzania.

Katika kikosi cha wanariadha 90 watakaochuana na Failuna, iwataja Wakenya, Ruth Chepngetich na

Brigid Kosgei ndiyo wenye rekodi kali ambao kama Failuna ataamua kupambana nao, hata akishindwa basi atakuwa na uhakika wa medali ya tatu ya shaba.

Failuna amekiri kuwa nyota hao ndio wanampa presha katika orodha ya wanariadha watakaochuana Jumamosi.

“Rekodi zao ni bora zaidi ya za kwangu, ila kwenye ushindani lolote linaweza kutokea na inategemea na jinsi utakavyoamka siku hiyo, ila Mungu yupo nitapambana nao jino kwa jino hatua kwa hatua,” alisema.

Kosgei ndiye anashikiria rekodi ya dunia ya saa 2:14:04 aliyoiweka Oktoba 13 2019 katika mbio za Chicago Marathon na amewahi kuwa bingwa wa mbio London Marathoni mwaka 2019 na 2020.

Chepng’etich ana muda wa saa 2:17:01, akimuacha Failuna anayekimbia kwa saa 2:27:00 kwa dakika 10 na ni bingwa mtetezi wa mbio za dunia za Qatar za mwaka 2019.

Muingereza,Stephanie Twell ni miongoni mwa nyota wanaopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mbio hiyo kutokana na muda anaokimbia na uzoefu wake ambapo amewahi kuwa bingwa wa dunia mwaka 2008 na mshindi wa medali ya shaba kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2010 katika mbio za mita 1500 japo sasa amejikita kwenye marathoni.

Jana kocha wa timu ya Tanzania kwenye Olimpiki, Thomas Tlanka aliiambia Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Japan kwamba kama Failuna ataongeza juhudi katika mbio yake ana uhakika wa kurejea na medali yoyote ile.

“Tumeangalia viwango vya wapinzani, wakali ni wawili pekee wale Wakenya, wengi kwenye ‘starting list’ hawana uzoefu mkubwa wa marathoni, tumuombeeni Failuna awe salama naamini atafanya kitu,” alisema.

Kuhusu Simbu na Geay, kocha Tlanka alisema; “Hata wote wakiamua na kujipanga, Simbu yuko fiti sana na ni mzoefu.”