Rekodi zaibeba Simba Kirumba

Muktasari:

HESABU ya mechi tatu za Simba kufunga hesabu za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu inaanzia leo pale watakapokuwa na kibarua cha ugenini dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10 jioni.

HESABU ya mechi tatu za Simba kufunga hesabu za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu inaanzia leo pale watakapokuwa na kibarua cha ugenini dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10 jioni.

Ushindi wa leo dhidi ya Polisi Tanzania, utaifanya Simba kufikisha pointi 70 na hivyo kuhitaji ushindi katika mechi zake mbili zitakazofuata dhidi ya Mbeya City na Yanga ili itangaze rasmi ubingwa ambao utakuwa wa nne mfululizo kwake.

Matokeo hayo ya ushindi leo pamoja na ya hizo mechi mbili zitakazofuata baada ya hapo, yataifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 76 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu nyingine yoyote kwani Yanga walio nafasi ya pili na pointi zao 64, watamaliza wakiwa na pointi 73

Kwa upande mwingine, wenyeji Polisi Tanzania wanalazimika kuibuka na ushindi katika mechi ya leo, ili wafikishe pointi 44 ambazo zitawafanya waweke hai matumaini yao ya kumaliza kwenye nafasi nne za juu na kungalia uwezekano wa kushirikiKombe la Shirikisho msimu ujao.

Simba imekuwa na historia ya kufanya vyema mbele ya Polisi iliyopanda Ligi Kuu msimu uliopita kwani imebuka na ushindi mara zote tatu walizokutana, ikifunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Polisi wanaikaribisha Simba huku wakiwa na takwimu zisizovutia pindi wanapokuwa uwanja wa nyumbani katika mechi za hivi karibuni na uthibitisho wa hilo, katika mechi 10 zilizopita nyumbani, wameibuka na ushindi mara tatu tu, kutoka sare nne na kupoteza michezo mitatu wakifunga mabao saba na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara saba.

Lakini kiujumla pia wamekuwa hawana mwendenendo mzuri kwani katika mechi 10 zilizopita za Ligi Kuu walizocheza nyumbani na ugenini, wamepata ushindi mara nne, sare nne na wamepoteza mbili.

Hali ni tofauti kwa Simba ambao wamekuwa moto wa kuotea mbali kwenye Ligi Kuu sio tu kwa mechi za ugenini bali hata zile za nyumbani ambapo katika mechi zao 10 zilizopita wameibuka na ushindi mara tisa na kutoka sare moja na wamefunga mabao 23 huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tatu.

Ubabe huo wa Simba ni hata katika mechi za ugenini ambapo katika mechi 10 zilizopita, wameibuka na ushindi mara tisa na kutoka sare moja, wakiwa wamefumania nyavu mara 22 na kufungwa mabao matatu.

Kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa alisema wanafahamu mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na wapinzani walivyo, lakini kwa maandalizi waliyoyafanya wana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi

“Mchezo hautakuwa mwepesi kwa sababu wapinzani wana timu nzuri, lakini kwenye mazoezi yetu tumeelekeza nguvu kwenye kufunga mabao, lengo ni kuona tunatumia vyema nafasi tutakazopata.

Kikosi nilichokuja nacho wote wako vizuri kwa ajili ya mchezo huo, lakini niseme licha ya rekodi tuliyonayo kwa wapinzani hao, hatuwezi kuwabeza kwani mpira huwa na matokeo tofauti” alisema Gomes.

Kwa upande wa Polisi Tanzania, kocha wao msaidizi George Mketo alisema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi licha ya ubora wa wapinzani wao.

“Itakuwa ni siku nyingine na uwanja mwingine kwahiyo ishu ya rekodi hatuipi nafasi, kimsingi tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi hiyo vijana wako fiti wakingoja muda tu

Kazi iliyobaki ni ya wachezaji 11, tunawaheshimu Simba kwa sababu ni timu kubwa na bora Afrika lakini tumejipanga kucheza kusaka ushindi ili kufukuzia nafasi nne za juu” alisema Mketo.