Rekodi za Kuvunjwa Kariakoo Dabi

Muktasari:

BAADA ya tambo nyingi mitaani za watani wa jadi, Simba na Yanga, mchezo wa Leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, ndio utaamua nani mwamba kati yao msimu huu.

BAADA ya tambo nyingi mitaani za watani wa jadi, Simba na Yanga, mchezo wa Leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, ndio utaamua nani mwamba kati yao msimu huu.

Mchezo huo unaogusa hisia za wengi ndani na nje ya nchi, mbali na matokeo yanayosubiriwa na wengi, pia kuna rekodi zilizowahi kuwekwa za mechi ya watani na hadi sasa hazijavunjwa.

Hizi hapa rekodi hizo tamu zinazozitesa timu hizo.

HAT-TRICK YA KING KIBADENI

Rekodi hii haijavunjwa hadi sasa. Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni alifunga mabao matatu katika mechi ya watani iliyochezwa Julai 19, mwaka 1977.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda bao 6-0, Kibadeni akifunga mabao matatu dakika ya 10, 42 na 89 na mengine yalifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti’ (mawili) na Selemani Sanga.

KICHUYA

Oktoba Mosi, 2016 Simba walikutana na Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa na siku hii itakumbukwa kwa bao tamu la Shiza Kichuya la kusawazisha akipiga mpira wa kona ulioenda moja kwa moja wavuni.

Mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Simba ilisawazisha dakika za jioni kutokana na kona hiyo mpira uliomshinda kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez’.

Yanga ilitangulia kupata bao kipindi cha kwanza lililofungwa na Amissi Tambwe, kabla ya mambo kugeuka.

MABAO 3-3

Mechi hii iliyochezwa Oktoba 20, 2013 ilimalizika kwa matokeo ya kushangaza hasa kwa mashabiki wa Yanga kuamini tayari wamepata ushindi na kipindi cha kwanza walitoka kifua mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa na Mganda Hamis Kiiza aliyefunga mawili.

Waliamini wanakwenda kulipa kisasi cha mabao 5-0, waliyofungwa na watani zao miaka miwili iliyotangulia.

Hata hivyo, kipindi cha pili Simba ilisawazisha mabao hayo kupitia Joseph Owino, Bertram Mwombeki na Gilbert Kaze.

Mechi hii iliweka rekodi ya Simba na Yanga kufungana mabao mengi kila kipindi.

USHINDI MKUBWA

Rekodi nyingine ya miaka ya hivi karibuni ambayo inasubiriwa kwa hamu kuvunjwa ni ile iliyowekwa Mei 6, 2012 walipokutana miamba hiyo miwili ya soka nchini.

Katika mchezo huo uliokuwa wa kukamilisha ratiba kwani Simba walikuwa wametwaa ubingwa tayari waliweka rekodi ya kuifunga Yanga mabao 5-0 kwa mabao ya Emmanuel Okwi (mawili), Felix Sunzu, kipa Juma Kaseja na marehemu Patrick Mafisango.

Kipigo hicho kilikuwa kikubwa kwa Yanga tangu walivyopigwa tena 6-0, mwaka Julai 19, 1977, walipokuwa wakilipa kisasi cha kupigwa mabao 5-0 na Yanga kwenye mchezo wao uliochezwa Juni 1, 1968.

DAKIKA ZA JIONI

Mshambuliji wa Yanga, Kenneth Asamoah ni miongoni mwa wachezaji walioweka rekodi katika mechi ya watani akifunga bao dakika za jioni.

Katika fainali ya Kombe la Klabu Bingwa wa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame) iliyochezwa Julai, 10, 2011, Yanga walishinda bao 1-0. Asamoah alifunga bao hilo dakika ya 109 akimalizia krosi ya Rashid Gumbo mchezo uliochezwa kwa dakika 120.

KIPA KUTUPIA NYAVUNI

Ni katika mechi ya ushindi wa mabao mabao 5-0 Simba ikishinda, iliwekwa rekodi nyingine kwa kipa kufunga bao na hadi sasa hakuna aliyeifikia.

Kaseja alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti akifuata nyayo za aliyewahi kuwa kipa wa Simba, Idd Pazi ‘Father’ mwaka 1985.

Katika mechi hiyo Kaseja alifunga bao la nne kwa penalti akimtungua kipa, Said Mohammed ‘Nduda’ kabla ya baadaye marehemu Mafisango kufunga hesabu kwa bao la tano.

MABAO SABA

Katika miaka ya hivi karibuni rekodi nyingine iliyopo na haijavunjwa mpaka sasa ni ile mechi ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa mabao saba kutupiwa nyavuni.

Ilikuwa ni mechi ya ligi iliyopigwa Aprili 18, 2010 na Simba ilishinda mabao 4-3 kwa mabao ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ aliyefunga mawili, Uhuru Selemani na Hillary Echesa.

Yanga ilipata mabao yake matatu yaliyofungwa na Jerry Tegete aliyefunga mawili na Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye kwa sasa hachezi ligi.