Ramadhani Singano, ilivyokuwa Mazembe mpaka Nkana Fc
MAZINGIRA yana nafasi kubwa ya kutengeneza ndoto za mtu baadaye, ukitaka kuamini hilo, muulize Mtanzania Ramadhan Singano ‘Messi’ anayecheza Nkana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia (MTN).
Hakukurupuka kuingia kufanya kazi ya soka, ni kitu ambacho kilikuwepo kwenye familia yake. Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Messi, ambaye amesimulia namna alivyokuwa akiwaona kaka zake wakicheza soka na hapo akapata mzuka na kuwafuata kila wanapokwenda kucheza mechi.
“Mazingira ya familia ndio sababu ya kucheza soka ndio maana inaweza kuwa ngumu ukiniuliza isingekuwa soka ningefanya kazi gani, nilikuwa natoroka shule ili mradi tu nikacheze,” anasema ambaye amewahi kuzichezea Simba na Azam.
MAISHA YA TP MAZEMBE
Anafichua faida za kutoka nje ya mipaka ya Tanzania jinsi kunavyotafsiri kiwango chake, kujua thamani yake, kujifunza ni vitu gani anatakiwa kuvifanya ili kufaidi matunda ya kipaji.
“Japokuwa TP Mazembe sikupata nafasi ya kucheza kutokana na ushindani wa namba kwa wachezaji niliowakuta, pamoja na hilo akili yangu imefunguka kutambua mimi ni nani. Hilo limetokana na aina ya maisha niliyoyakuta kwa wachezaji wa DR Congo, mitazamo yao ya kazi na maisha kwa ujumla,” anasema Singano na anaongeza kuwa,
“Mfano mzuri ni Robert Kidiaba, alikuwa kipa wa TP Mazembe na sasa ni Waziri wa Michezo wa DR Congo, cheo ambacho ni kikubwa kabisa. Alikuwa mwanasoka na sasa ameaminiwa na Serikali kutokana na jinsi ambavyo alijipa thamani ya mtazamo na kile anachokifanya,” anasema.
Anaendelea kusimulia kwamba amebahatika kukaa na Kidiaba aliyekwenda kuwasalimia kwenye kambi yao baada ya kusikia Watanzania wamejiunga na TP Mazembe, fursa hiyo anakiri ilimfunza mengi.
“Alikuja kutusalimia na kutuambia Watanzania kwake ni kama ndugu kutokana na Mbwana Samatta kucheza timu hiyo. Alitushauri jinsi ya kuyachukulia mambo tukiwa uwanjani na maisha ya kawaida, ndipo nikajua mitazamo ya wenzetu ipoje.
“Mbali na Kidiaba niliona wachezaji wengine jinsi wanavyoishi, wanachojadili wakikutana, kiukweli najiona nina hatua kubwa, itakayonisaidia katika mapambano yangu mengine,” anasema.
Ukiachana na mafunzo aliyopata, anasimulia usajili wake kwamba ulisimamiwa na wakala wake, aliyemwambia anatakiwa kusaini klabu hiyo, akitokea Azam FC.
“Sikutaka kulaza damu baada ya kuambiwa kuwa natakiwa TP Mazembe, kwani ni timu kubwa licha ya kutocheza mechi, nimejifunza vingi mazoezini na nje ya hapo na bado ninajifunza,” anasema.
KUTUA NKANA
Singano anasema ilikuwa shauku yake kupata timu ya kucheza baada ya kujifunza vitu vya kiufundi ndani ya Mazembe ambako alikuwa hana namba kwenye kikosi cha kwanza, ndipo alijiunga na Nkana kwa mkopo wa mwaka mmoja.
“Nilitamani kile nilichojifunza TP Mazembe nikiingize kwenye matendo, ili nikicheza na kufanya vizuri niwe na mchango kwenye timu ya Taifa kama ilivyo kwa wachezaji wengine,” anasema.
Nje na hilo Singano anasema anapambana ili awe sababu ya wengine kufuata nyuma yake kucheza soka la nje.
“Ninachoweza kuwashauri wachezaji wenzangu, wajitoa kusaka heshima yao kwa kukubali changamoto mpya nje ya mipaka yao. Mfano mzuri ni Samatta na Simon Msuva ambao wamejipa thamani ya kuachana na mazoea ya ndani na kwenda nje,” anasema Singano.
Anawaondoa shaka kwamba wasiogope kufeli akiamini ni moja ya hatua kuthubu, kuliko kuishia kucheze soka la Tanzania, wakati wana uwezo na malengo makubwa.
“Jambo lingine linalowatesa wachezaji wengi wanahofia kushindwa, vipo vingi nyuma yao vinavyowakatisha tamaa, wajitoe kutesekea malengo yao, kuliko kutesekea watu. Hilo halitawasaidia kwani hayo ni maisha yao binafsi,” anasema.
ABDUL AMFARIJI
Singano anasema amekutana na beki wa zamani wa Yanga, Juma Abdul anayecheza klabu ya Indeni FC, jambo lililompa faraja kuona wapo Watanzania wawili wanaopambana.
“Mechi ya kwanza tumecheza na timu ya akina Abdul aliingia kipindi cha pili, baada ya mchezo tulikaa na kuzungumza mawili matatu, kiukweli alifurahi na nilifurahi pia, naamini kila kitu kitaenda sawa na tutakuwa mabalozi wazuri,” anasema.
MAFANIKIO, UVUMILIVU
Singano anasema japokuwa ndio kwanza ameanza kazi Nkana, lakini safari yake haikuwa rahisi, ndani yake ilitawaliwa na uvumilivu wa kuzipokea changamoto kwa muono mzuri, zilizompa hatua aliyonayo sasa.
“Soka bila uvumilivu, hakuna mafanikio, binafasi nimepitia mengi lakini nilikuwa namuomba Allah anipe wepesi na mimi sio mtu wa kuzungumza sana, yakapita maisha mengine yanaendelea,” anasema na anaongeza kuwa:
“Soka lipo kwenye damu kwa sababu nilikuwa naona kaka zangu wakicheza, nakumbuka nikiwa mdogo nilikuwa natoroka shule kwenda kufanya mazoezi, nilipigwapigwa sana na waalimu, lakini sikukata tamaa ya kutetea ndoto yangu,” anasema.
SIMBA, AZAM
Singano alijiunga na Simba 2011 na 2015 alihamia Azam FC, alikotokea kwenda kusaini TP Mazembe, anasema hizo timu zimemsaidia kumjenga na kumpa hatua kubwa ya maisha yake ya soka.
“Kwa nyakati tofauti zimenijenga, zimeacha alama katika maisha yangu, hivyo sitaweza kuzisahau kwa hatua niliyopiga, ingawa siwezi kuingia kiundani kuweka vitu vyote wazi,” anasema.
ASICHOSAHAU
Singano anakumbuka akiwa mdogo alikuwa anakwenda na wenzake majalalani kuokota mikaa, kisha akiikusanya mingi anapeleka kwao, wakati mwingine anauza ili kupata fedha.
“Ujue mambo ya utoto ni mengi, tunakwenda ambako gari la mkaa limeshuka, tunaokota iliobaki, wakati mwingine mpaka majalalani, kifupi nimepitia mengi lakini nashukuru Mungu hapa nilipo sasa,” anasema.
Ukiachana na hilo Singano anasema kitu kingine ambacho hakiwezi kukisahau ni wazazi wake ambao, hawapo duniani kwa sasa na kutamani wangekuwepo angalau wangeonja kidogo kile anachokipata kwa sasa.
“Wazazi wangu walifariki muda mrefu, huwa nawakumbuka lakini huwa napenda kutanguliza shukrani kwa Mungu, natambua wote ni wapitaji na kila mtu kaandikiwa muda wake,” anasema.
WAMEZALIWA SITA
Anasema yeye ni mtoto wa mwisho kati ya sita, wamefariki wawili, wamebakia wanne, ambao ni Khamis, Moghammed na Bakari.
“Kaka zangu hao wamekuwa faraja kubwa kwangu, wakati mwingine kama kuna jambo linanisumbua, nikianza kulia huwa wananiambia ninyamaze, nimshukuru Mungu na natakiwa kupambana kwa kadiri ninavyoweza ili niweze kuishi maisha bora,” anasema.
AKISTAFU SOKA
Anasema ndoto yake kubwa akistaafu ni kuwa mfanyabiashara na tayari anauza fulana, lengo lake anataka kuyajenga maisha yake ya baadaye ili asije akaanza kusumbuka.
“Kuna maisha baada ya soka, ndio maana najiwekea akiba ya namna ya kuishi nikimaliza kazi uwanjani, siwezi kujisahau kuna haya ndio maisha mpaka mwisho,” anasema.
AANZA NA TAJI
Licha ya ugeni wake kwenye klabu hiyo, Singano ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kukisaidia wikiendi iliyopita kuanza na taji la ufunguzi wa msimu mpya wa MTN.
Singano alicheza dakika 90 za mchezo huo na kumpoteza Mtanzania mwenzake Abdul, ambaye anaichezea Indeni. Nkana waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku akishuhudiwa winga huyo akigongesha nguzo.
“Nimefurahia kuanza kwa kupata ushindi na medali, imefungua njia kwangu kuelekea msimu mpya,” anasema.
AKUMBWA NA MSIBA
Mara baada ya mchezo wa ufunguzi wa msimu, chama jipya la Singano lilipatwa na msiba wa kiungo wao, Chrispin Mulenga maarufu kama Wado nchini humo, ambaye alipata ajali ya gari.
“Nakumbuka kuwa aliingia kipindi cha pili lakini yote ni mapenzi ya Mungu hatuna budi kumshukuru kwa yote.”
KUONJA UTAMU KIMATAIFA
Singano atakauwa Mtanzania wa pili kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na klabu hiyo yenye maskani yake Kitwe, Zambia ambapo wa kwanza alikuwa Hassan Kessy, ambaye kwa sasa amerejea nchini na kukipiga Mtibwa Sugar yenye maskani yake Marogoro, inayoshiriki Ligi Kuu Bara.