Polisi wawatuliza mashabiki Yanga

Mashabiki wa Yanga wakilalamika baada ya muda wa mechi yao dhidi ya Simba kusogezwa mbele. Picha na Michael Matemanga

SIMBA na Yanga zimeteka hisia za Watanzania na zimewagawanya pande mbili kuzishabikia, hilo linawafanya mashabiki kujitoa kikamilifu kuzipa sapoti pindi zinapokuwa na majukumu.

Leo muda wa saa 1:00 usiku, zinacheza mechi ya mzunguko wa pili, baada ya raundi ya kwanza zikitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1, Yanga alifunga Michael Sarpong kwapenalti na Simba ni Joash Onyango kwa kichwa.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa 11:00 kabla ya mabadiliko ya saa 1:00 jioni, jambo ambalo limeonekana kuwachefua mashabiki wa Yanga.
Mashabiki wa Yanga walishuka kutoka uwanjani na kwenda chini wakileta taharuki na kupinga muda huo.
Jambo ambalo maaskari wa kutuliza ghasia waliingilia kati kuondosha mlundikano wa mashabiki hao.
Lakini kwa upande wa mashabiki wa Simba baadhi ambao walikuwa chini walikuwa wanaendelea na mambo yao.
Pamoja na changamoto hiyo ya muda, mashabiki hao hawajakata tamaa yakuondoa uwanjani kuzishabikia timu zao.