Polisi: Simba haihusiki na kujinyonga kwa Mwambene

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Christina Musyani

Muktasari:

  • Katika mchezo huo ambao ulipigwa saa 10:00 jioni katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wenyeji waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limekanusha kuwa tukio la Khalfan Mwambene (17) mkazi wa Karobe jijini hapa aliyekutwa amejinyonga Januari 17 haihusiani na matokeo ya mchezo baina ya Mbeya City na Simba kama ilivyosambazwa mitandaoni, huku likitoa angalizo kwa wananchi kutoa taarifa rasmi kwenye vyanzo husika kabla ya kuhabarisha habari zisizo na ukweli na kuleta taharuki.

Katika mitandao ya kijamii imeeleza kuwa kijana huyo alijinyonga kufuatia Simba kupoteza mchezo wake dhidi ya Mbeya City kwa bao 1-0, huku akiacha ujumbe kuwa 'Naipenda Simba na nizikwe na jezi ya Simba'

Akizungumza na Mwanaspoti leo Januari 19 mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Christina Musyani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema marehemu alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua akiwa kwenye zizi la Ng'ombe.

Amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika, ambapo Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi, akibainisha kuwa tukio lilitokea saa 1:30 asubuhi na siyo baada ya mechi hiyo akieleza kuwa taarifa za mitandaoni hazina ukweli wowote.

"Nashangaa tukio lilitokea asubuhi, mpira ukachezwa jioni je marehemu alijuaje kwamba Simba atafungwa hadi kujinyonga? Amehoji na kusema

"Kijana huyo alikuwa anachunga Ng'ombe ambapo alikutwa amejinyonga kwa kamba ya chandarua, bado tunaendelea na uchunguzi, niwaombe hao wanaosambaza taarifa za uongo kuacha mara moja, watafute vyanzo vya uhakika ili kuondoa taharuki kwa jamii" amesema Christina.

Kamanda huyo pia amethibitisha kutokea tukio la Mwalimu wa Shule la Msingi, Kambarage ya jijini hapa ambaye alikutwa amejinyonga akieleza kuwa bado naye chanzo hakijajulikana na Jeshi la Polisi linaendelea kufuatilia kwa undani sababu za tukio hilo.

"Niwaombe wananchi kuwa wawazi hata kwa familia zao wanapokuwa na tatizo lolote ili kushauriwa, lakini pia kujichukulia sheria mkononi ni jinai, nchi yetu inaongozwa na sheria, jamii ibadilike ithamini utu kwanza kwani hata Mungu hapendi mtu kuua au kujiua" amesema Kamanda huyo.

Uongozi wa klabu ya Simba umetoa salamu za rambirambi kwa familia hiyo kufuatia kifo cha Mwambene.

"Khalfani ameonyesha mapenzi makubwa kwa Simba, tunamuomba Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi,"