Phiri, Inonga waiwahi Coastal Union

MASTAA wawili wa Simba, Moses Phiri na Henock Inonga wamerejea  mazoezini leo  baada ya kuwa nje ya uwanja tangu Desemba mwaka jana kutokana na kuwa majeruhi.

Phiri aliumia misuli ya miguu katika mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyofanyika Desemba 21 kwenye uwanja wa Kaitaba Bukoba wakati Inonga alipata majeraha katika mchezo dhidi ya Prisons uliofanyika Desemba 30 kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mchezaji mwingine aliyerejea leo ni Peter Banda ambaye nae  alikaa nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu Novemba 9 mwaka jana baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mchezo dhidi ya Singida Big Stars.

Phiri mwenye mabao 10 alikosa michezo minne ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, Prisons, Mbeya City na Dodoma Jiji pamoja na ile ya kirafiki katika kambi ya wiki moja waliyoweka Dubai  hivi karibuni wakati Inonga alikosa michezo miwili dhidi ya Mbeya City na Dodoma Jiji.

Wachezaji hao leo Jumatano Januari 25 wameonekana wakifanya mazoezi vizuri kwenye uwanja wa MO Simba Arena Bunju na wakiwa fiti.

Mazoezi ya timu hiyo ambayo yalianza kwa kocha Juma Mgunda kuwataka  wachezaji kukimbia kwa dakika kadhaa kuzunguka uwanja ili kupasha misuli moto kabla ya baadae kugawa  wachezaji katika makundi manne  na kutakiwa  kukimbia kwa kasi kuanzia goli la kwanza hadi la upande mwingine.

Wachezaji hao walionekana kumudu  mazoezi yote hayo kwa ufasaha na kisha kuingia katika mazoezi ya kuchezea mpira.

Baada ya kufanya mazoezi hayo kwa zaidi ya dakika 30, Phiri alitoka nje ya uwanja  na kuendelea na mazoezi ya peke yake chini ya kocha wa viungo wakati wenzie wakicheza mechi ya nusu uwanja.

Kocha msaidizi wa Simba, Juma Mgunda alisema kurejea kwa wachezaji hao ni faraja kwao na kucheza mechi ijayo dhidi ya Coastal Union  itategemea na  maendeleo yao kwa siku tatu zilizobaki.

Msemaji wa Simba, Ahmed Ally amesema wamefurahi kurejea kwa wachezaji hao kwani watakiongezea nguvu kikosi hicho kuelekea mechi ijayo ya Kombe la Azam Shirikisho dhidi ya Coastal Union itakayofanyika Jumamosi.