Pamba yakubali yaishe, Geita Gold hiyooo VPL

Muktasari:

Kwa matokeo hayo, Pamba na Transit Camp watashiriki hatua ya play off kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao baada ya kumaliza ligi daraja la kwanza katika nafasi ya pili na tatu kwenye kundi lao B.

Mwanza. Licha ya ushindi wa bao 1-0 walioupata Pamba dhidi ya Transit Camp haujaisaidia moja kwa moja timu hiyo kupanda Ligi Kuu, huku matumaini yakibaki kwenye hatua ya mchujo 'play off'.

Kabla ya mchezo wa leo Jumamosi wa kuhitimisha ligi daraja la kwanza kundi B, Pamba ilihitaji pointi tatu lakini ikiiombea Geita Gold wapoteze ili waweze kukaa usukani, hesabu ambayo imekwama.


Pamba kwa matokeo ya leo imefikisha pointi 36 wakizidiwa na Geita Gold pointi moja kufuatia  ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate na kujihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao wakiungana na Mbeya Kwanza kutoka kundi A waliopanda mapema kabla ya mechi tatu.

Katika mchezo wa leo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Pamba ilionekana kuwa na presha kubwa ya kuhitaji ushindi huku Transit Camp wakicheza kwa utulivu na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika kwa suluhu.

Pamba walijitahidi na dakika ya 81 Said Zae akaiandikia bao la ushindi na kuwaamsha mashabiki waliokuwa uwanjani hapo na sasa hesabu zao kuelekezwa katika play off kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Wakati huohuo, Rhino Rangers ya mjini Tabora ambayo iliwahi kucheza Ligi Kuu kabla ya kushuka msimu wa 2012/13 wamejikuta wakishuka daraja licha ya ushindi walioupata dhidi ya Kitayosce wa mabao 2-0 na kuungana na Mbao, Alliance na Singida United walioshushwa mapema katika kundi B.