Pablo: Kila mtu ashinde zake

BAADA ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-1, dhidi ya Ruvu Shooting, Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco amesisitiza kwamba; “Kila mtu ashinde zake”

Ameweka wazi kutokata tamaa na mbio za ubingwa huku kauli hiyo ikichagizwa na mwenendo wa washindani wao Yanga ambao kwenye mechi tatu mfululizo walisuluhu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Pablo alisema wanacheza mechi moja baada ya nyingine pasipo kuangalia ya watu wengine na amewaambia hilo wachezaji wake na wamemuelewa.

“Bado hatujakata tamaa na tunachokizingatia ni kushinda kila mchezo, hatuwezi kuwafikiria wapinzani wetu kwani kwa kufanya hivyo itatutoa kwenye malengo ambayo tumejiwekea,” alisema Pablo na kuongeza:

“Jambo kubwa ni utayari kwa ajili ya mechi zetu na kuona kila mchezo unakuwa na mpango tofauti ili kuhakikisha tunapata ushindi na hilo litatufanya tuweze kuwa kwenye sehemu nzuri mwishoni wa msimu.

“Hii mechi ni ngumu, ratiba imebana sana. Muda wa mechi na mechi ni mfupi sana lakini hakuna namna, hakuna kisichowezekana tutapambana kuhakikisha tunafanya kilicho sahihi kwa kutumia mbinu sahihi kufurahisha mashabiki wetu.”

Simba itakuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa leo saa 1 usiku kucheza na Kagera Sugar ikiwa ni mchezo wa kisasi kwa Simba baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Januari 26, 2022, katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kufungwa bao 1-0.

Bao hilo la Kagera lilifungwa na mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Hamis Kiiza ‘Diego’ kabla ya nyota huyo kupewa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga mpira kwa makusudi huku mwamuzi Hussein Athuman alishapuliza kipenga.

Simba inaingia kwenye mchezo huu ikiwa nafasi ya pili na pointi 46, Kagera Sugar ikiwa ya sita na pointi 26, baada ya timu zote kucheza michezo 22.

Kitendo cha Yanga kupata suluhu dhidi ya Prisons kimefanya kuwe na gepu la pointi 11, Yanga ikiwa na pointi 57 huku Simba ikiwa na pointi 46.

Kwenye mchezo wa leo kama Simba itashinda basi itafikisha pointi 49 na kufanya kuwe na tofauti ya pointi nane wote wakibakiza mechi saba Ligi kuisha.


H2H ZAO

Kagera 0-3 Simba

Simba 1-0 Kagera

Simba 2-0 Kagera

Kagera 0-2 Simba

Kagera 1-0 Simba


MECHI ZINGINE LEO

Polisi itacheza na Dodoma Jiji mkoani Kilimanjaro saa 8 mchana huku timu hizo zikiwa na rekodi za sare mbili kwenye mechi zao mbili za mwisho. Coastal Union wataikaribisha Biashara Jijini Tanga saa 10:00 jioni  kwenye mechi ambayo mara ya mwisho mwenyeji alishinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Polisi, Dodoma, Biashara na Coastal Union bado zipo kwenye nafasi ambayo lolote likitokea zinaweza kushuka daraja kwani pointi zinakaribiana baina ya timu mbalimbali kwenye msimamo huo unavyosomeka sasa.