Onyango: Hili trela tu, filamu inakuja

BEKI wa kati wa Simba, Joash Onyango amesema msimu uliopita ameamua kuonyesha kiwango bora kutokana na baadhi watu kumbeza na kumuita ‘Babu’ na kudai hii ni trela tu na filamu yenyewe inakuja kwa msimu ujao.

Onyango alisema amekuwa akiona maneno mengi kutoka katika maeneo tofauti ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii ambayo kuna baadhi ya mashibiki wakisema Simba imesajili mzee.

Alisema kiwango ambacho ameonyesha msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao amepanga kufanya hivyo zaidi kutoka na sababu mbili.

“Nafahamu wale ambao walikuwa wananibeza na kuniita mzee sasa wengi wao wapo kimya na msimu ujao kama nikiendelea kuwa mzima nitawazima kabisa na kuacha kufanya hivyo,” alisema Onyango na kuongeza;

“Sababu nyingine nataka kuona Simba inafanya vizuri katika mashindano yote kwa maana hiyo nimejipa zaidi kuonyesha kiwango bora ili kuisaidia timu kufikia malengo yake ambayo imejipangia.

Ikiangalia vizuri muonekano wangu wa sasa utaniona nimeweka nywele rangi nyeupe kama mzee ili kuwajibu wale ambao walinibeza sasa nahitajika kupewa heshima.”

Onyango alisajiliwa na Simba msimu uliopita kwa mkataba wa miaka miwili akitokea, Gor Mahia ya Kenya.