Okrah, Okwa gari limewaka! Zoran atajwa

Okrah, Okwa gari limewaka! Zoran naye yumo

Klabu ya Simba usiku wa jana imeibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo kirafiki dhidi ya Malindi kwenye uwanja wa Amaan, Zanzibar. Lakini kubwa zaidi mastaa wa timu hiyo Mghana Agustine Okrah na Mnigeria Nelson Okwa kurejea kwenye viwango vyao jambo lililolipa mzuka benchi la ufundi chini ya kocha Juma Mgunda.
Okwa na Okrah walisajiliwa mwanzoni mwa msimu huu wakibeba matumaini ya Simba japo hawakuwa na mwanzo mzuri kutokana na mazingira mapya na mabadiliko ya makocha lakini sasa unaambiwa gari limewaka wakirudi na moto.
Okwa anayemudu kucheza kiungo wa kati, ushambuliaji na winga zote mbili taarifa za kuaminika lilizo nazo Mwanaspoti alikatishwa tamaa na kocha Zoran Maki aliyeondoka Simba kutokana na kutompa nafasi ya kuonyesha makali, lakini chini ya Mgunda amerudi kwenye kasi na sasa anasikilizia mechi za mashindano zianze aanze kukiwasha.
Hali hiyo ipo pia kwa Okrah aliyekuwa anaanzia benchi chini ya Zoran aliyedaiwa aliwakataa mastaa wengi akiwemo kinara wa mabao Moses Phiri, beki Joash Onyango na kiungo mwingine Mnigeria, Victor Akpan ambao kwa sasa wameanza kufanya vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema moto wa mastaa hao umezidi kukolea kambini na sasa ana kikosi kipana kinachompa nafasi ya kumpanga yeyote na kumpa matokeo ya ushindi na burudani.
Mgunda alisema utajiri wa wachezaji walio katika viwango bora kwenye kila eneo ni jambo linalomuumiza kichwa ampange nani na kumuacha nani.
“Kuna wachezaji hawakuanza vizuri msimu na wengi ni kutokana na mazingira kuwa mapya mfano Okwa, Dejan (Georgijevic) na Okrah, lakini sasa wote wamerejea kwenye ubora wao kwa asilimia kubwa na kila mmoja yupo tayari kuipa matokeo chanya Simba,” alisema Mgunda aliyetua klabuni hapo akitokea Coastal Union na kuingoza kwenye mechi tatu za mashindano na kushinda zote.
“Eneo la kiungo wa chini pia limepigiwa kelele na watu wengi na sisi kama benchi la ufundi tuliona kuna tatizo na tayari tumelifayia kazi. Kanoute (Sadio), Mkude (Jonas) na wengine wote tumewaeleza nini wanatakiwa kufanya pia tumeongeza mbinu  katika eneo hilo na tunaamini matatizo ya mwanzo tumeyapatia dawa,” alisema Mgunda, nyota wa zamani wa kimataifa wa Coastal na Taifa Stars.
Simba ikimaliza mechi ya pili ya kirafiki Jumatano ijayo dhidi ya Kipanga itarejea Dar es Salaam kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kwenda Angola kuumana na Primiero de Agosto katika pambano la kwanza la raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba na Agosto hazijawahi kukutana hata mara moja na viongozi wa mnyama tayari wameanza maandalizi ya kuhakisha wanaiondosha mapema tu Waangola hao na kutinga makundi huku lengo lao kuu kwa msimu huu kwenye michuano hiyo ya CAF ni kufika nusu fainali.