Nyosso, Kibaya wakabidhiwa Yanga

Mbeya. Wakati Ihefu ikiwavaa Yanga dakika chache zijazo, kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mwambusi amekiamini kikosi kilichoanza mechi iliyopita dhidi ya Geita Gold kumaliza kazi leo akiikabili Yanga.

Pia wachezaji walioanza wengi wanajivunia uzoefu walionao kwenye ligi kuu, huku wengine wakikipiga Yanga, Azam na timu nyingine ikiwamo Mtibwa Sugar.

Mchezo baina ya timu hizo unatarajia kupigwa uwanja wa Highland Estate wilayani Mbarali mkoani hapa, ikiwa ni mechiya kwanza kuwakutanisha wapinzani hao katika uwanja huo.

Pia ni mchezo wa tatu kwa timu hizo kukutana, ambapo Yanga imeshinda zote bila kujali nyumbani na ugenini, hivyo leo itakuwa ni kuendeleza au kuvunja rekodi.

Katika mchezo uliopita Ihefu ikicheza ugenini kwenye uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita, ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Geita Gold ikiwa ni kipigo cha tisa kwa timu hiyo na kubaki mkiani kwa pointi nane.

Kikosi cha leo dhidi ya Yanga, Mwambusi amewapanga nyota walewale ikiwa ni kipa Fikirini Mapara, Nico Wadada, Hassan Mwasapili, Juma Nyosso, Leny Kissu, Samuel Onditi, Raphael Daud ‘Loth’, Never Tigere, Joseph Mahundi, Peter Mwalyanzi na Jafari Kibaya.

Wanaosubiri benchi ni Shaban Kado, Mwaita Gereza, Isah Ngoah, Said Makapu, Ally Ally, Joseph Kinyozi, Ally Rmadhan ‘Oviedo’ Andrew Simchimba na Kitenga.