Ntibazonkiza ni balaa jingine Simba

SAIDO Ntibazonkiza ameonyesha kwamba  anaweza kuwa msaada kwenye kikosi cha Simba kufuatia kutupia mabao matatu 'hat trick' kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi akiwa na timu hiyo dhidi ya Tanzania Prisons.

Ni kama mashabiki wa Simba walisahau kutokuwepo kwa mshambuliaji wao hatari, Moses Phiri ambaye ni majeruhi kutokana na kiwango cha nyota huyo aliyesajiliwa dirisha hili kutoka kwa wachimba madini wa Geita Gold.

Ntibazonkiza alitupia mabao matatu kwenye mchezo huo huku akitoa asisti moja kwenye ushindi wa mabao 7-1 ambao Simba imeupata dhidi ya Prisons na kufikisha jumla ya pointi 44.

Hizi ni dondoo muhimu za mchezo huo mabao Prisons ilimaliza pungufu kufuatia kwa  Samson  Mbangula kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Hennock Inonga.

Ntibazonkiza amekuwa mchezaji wa kwanza mpya msimu huu kufunga mabao matatu na kutoa asisti kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye ligi.

Hii ni mara ya kwanza msimu huu kufungwa hat trick mbili kwenye mchezo mmoja, mbali na Ntibazonkiza, John Bocco naye aliweka kambani mabao matatu kwenye nyavu za Prisons.

Ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza Simba ilipiga mashuti matano yaliyolenga lango huku Prisons ikipiga mawili.

Idadi ya mabao manane kufungwa kwenye mchezo mmoja ni idadi kubwa zaidi kushuhudiwa msimu huu.

Hiki ni kipigo kikubwa zaidi kwa Tanzania Prisons ambacho imekumbana nacho msimu huu wa 2022/23.

Ushindi huo umeifanya Simba kupunguza tofauti ya pointi baina yao na Yanga mabao wapo nyuma mchezo mmoja kutoka sita hadi tatu.

Simba imekuwa timu ya kwanza msimu huu kufunga mabao sita kwenye kipindi cha pili.