Ni Yanga na TFF Tena

Ni Yanga na TFF Tena

Muktasari:

Uongozi wa Yanga umelikumbusha Shirikisho la mpira wa miguu nchini(TFF) kutoa majibu ya kesi mbili zilizopo katika ofisi hizo.


UONGOZI wa klabu ya Yanga umelikalia kooni Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) likitaka watoe majibu dhidi ya kesi zao mbili zilizopo katika ofisi za Shirikisho hilo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa Novemba 20,Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema wao hawana tatizo na TFF, lakini wanashangaa kuona kesi zao zikichelewa kutolewa majibu kwa wakati mpaka sasa.

"Sisi hatuna tatizo na  TFF lakini kuna kesi ya Kabwili (Ramadhan) na tulipeleka hadi PCCB (Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa) hivyo tunawaomba TFF warejeshe majibu kwani huku sisi tulishapewa majibu.

Kesi ya Kabwili ilikuwa ni kuweka wazi kutaka kurubuniwa na baadhi ya viongozi wa soka huku sauti yake ikisambaa mitandaoni hali ambayo viongozi wa Yanga walisimama kidete kutaka jambo hilo lichunguzwe na yatolewe majibu.

Mwakalebela amesema suala la pili ambalo linawafanya washangae zaidi ni kuona kesi ya aliyekuwa mchezaji wao Benard Morrison kutopatiwa majibu ya kuwaridhisha.

"Kuhusu kesi ya Morrison,sisi tulizungumza wazi kwamba mkataba sio sahihi ni batili, tuliomba tupewe majibu lakini hatujapata mpaka leo.

"Wasiwasi wetu ni kwamba 15 Disemba dirisha dogo linafunguliwa hivyo wanaweza kubadilisha mkataba.Tunawaomba TFF waitishe kesi hii mapema kabla ya dirisha dogo kufunguliwa.

Pia tuna kesi CAS hivyo tunaomba suala hili lisikilizwe mapema ili hata huko usije ukaenda mkataba mwingine." amesema Mwakalebela.

Mwakalebela pia alizungumzia kuhusu propaganda za soka zinazoendelea huku akisema Yanga ni timu imara yenye viongozi imara na wafadhili imara ndio maana hawajapoteza mchezo mpaka sasa.

"Napenda niwahakikishie wapenzi wa Yanga kwamba msimu huu tumejipanga vizuri kuhakikisha tunachukua ubingwa. Hivyo kama wapo wenye uhakika wa tuhuma za kupanga matokeo au hujuma yoyote basi wajitokeze halafu wazungumze.Ukitaka kufanya vizuri unatakiwa uwe na viongozi bora, timu ikae kambini na sio kitu kingine."

__________________________________________________

 By THOMAS NG'ITU