Ni Derby ya Sakho, Aziz Ki

WAKONGWE wa Simba na Yanga hawapoi huko mtaani kuelekea kwenye dabi, kila mmoja anaipa tiketi timu yake kubwa kuliko ni wale wa Simba ambao wamefichua huu ndiyo mwanzo wa kurejesha mataji yote.

Hata hivyo, nyota hao wa zamani wa Simba na Yanga wameitaja dabi kuwa ya nyota wa kigeni, Aziz Ki na Pape Sakho katika vita ya ufungaji huku Yanga wakieda mbali wakisisitiza kwenye fowadi yeyote anakufunga.


Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’

Staa wa zamani wa Yanga anawaambia Simba wasiende uwanjani na matokeo ya Wiki ya Mwananchi, kwani yatawagharimu japo anakiri watani zao wana kikosi bora, lakini sio cha kuifunga Yanga.

“Ile mechi ya Wiki ya Mwananchi tulifungwa kwa makosa madogo tu, timu yetu ni nzuri na matokeo yale ilikuwa ni bahati mbaya tu, hivyo yasimpe Mnyama jeuri ya kuamini ndiyo yatajirudia Jumamosi, hilo wasahau,” ametamba Homa ya jiji.

“Yanga pale mbele yeyote anakufunga, kama sio Aziz Ki basi Mayele anakupa matokeo. Kule nyuma ukuta wetu uko imara kuanzia kwa kipa, beki Djuma Shaban yuko vizuri, pembeni kuna Lomalisa, katikati kuna Job na Mwamnyeto ingawa ikimpendeza kocha atafute mtu wa kuanza na Job, Mwamnyeto kama amekuwa mzito kidogo.

“Kocha akimuanzisha Bangala itakuwa kombinesheni nzuri na Job, Yanga itakuwa ni raha duniani,” anasema Makumbi anayesisitiza kuwepo uwanjani mapema.


Mtemi Ramadhan

Kiungo huyu msomi na fundi wa mpira wa zamani wa Simba anasema leo ndiyo safari ya timu yake kurejesha mataji moja baada ya jingine.

“Ni kweli timu zote mbili zimesajili vizuri kutokana na mahitaji na itakuwa dabi ya kusisimua zaidi, lakini kete yangu naiweka Simba,” anasema na kusisitiza kuwa Simba itacheza ikiwa na morali ya kutaka kurejesha mataji yote ambayo msimu uliopita yalichukuliwa na Yanga.

Mtemi amekitaja kikosi cha kwanza cha ubingwa Jumamosi kuwa ni Aishi Manula ambaye atasimama golini, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Inonga na Ouattara, katikati Chama na Mkude, Okrah, Sakho, Phiri na Okwa.


Sanifu Lazaro ‘Tigisha’

Nyota huyu aliyetingisha uwanjani akiwa Yanga anasema hii moja ya dabi ambazo anatarajia ziwe nzuri zaidi kwa timu hizo za Kariakoo.

“Japo naipa nafasi ya ubingwa timu yangu ya Yanga, lakini ni dabi ambayo itakuwa nusu kwa nusu kwa timu zote na ile yenye bahati ndiyo itaondoka na ubingwa, japo kete hiyo naiweka kwa timu yangu,” anasema Tingisha ambaye atakuwa mmoja wa wadau wa soka watakaokuwa kwa Mkapa, leo.


Fikiri Magosso

Beki wa kati wa zamani wa Simba, Fikiri Magossi anakwambia ni zamu yao kurudisha nyumbani Ngao ya Jamii, japo anakiri mechi kuwa ngumu kwa timu zote kutokana na ubora vikosi.

“Yanga wamefanya usajili wa ziada, lakini pia tumeona Simba imeacha wachezaji wao baadhi na kuingiza wapya kikosini. Zote zina vikosi vizuri, mwenye mpango mzuri ndiye atapata matokeo, japo naamini msimu huu ni zamu yetu,” anasema Magosso aliyewahi kutikisa enzi zake akikipiga Simba.

Anasema Simba mbali na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, imekuwa ikicheza pamoja hivyo yeyote atakayeanza atapeleka furaha Msimbazi.