NGUSI: Bao za tiktak, n'tafunga sana!

Monday October 11 2021
ngusu pic
By Saddam Sadick

WAKATI Ligi Kuu Bara ikisimama kwa muda, habari kubwa ilikuwa ni bao alilofunga staa wa Mbeya Kwanza, Crispin Mhagama ‘Ngushi’ na kuisaidia timu yake kuondoka na alama moja katika mechi hiyo.

Bao hilo alilolifunga kwa ustadi akipokea mpira wa juu na kufunga kwa ‘tiktak’ liliwaacha midomo wazi mashabiki na wadau wa soka hususani wapinzani wao Mbeya City waliokuwa wamejihakikishia ushindi.

Ngushi ambaye ndio mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu alifunga bao hilo lililoipa matokeo ya sare timu yake, hadi sasa mchezaji huyo ana mabao mawili sawa na Vitalis Mayanga wa Polisi Tanzania na Reliants Lusajo (Namungo).

Ngushi ameelezea maisha, mipango na mikakati yake kwenye soka, sambamba na nafasi ya Mbeya Kwanza mwisho wa ligi.

Alisema licha ya kuwa msimu wake wa kwanza, lakini uwezo anao wa kucheza soka na bao lake alilofunga dhidi ya Mbeya City walipotoka sare ya 2-2 haikuwa mara ya kwanza kwake kwani aliwahi kufunga bao kama hilo akiwa Boma FC wakati wakiizamisha Majimaji FC mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) uliopigwa wilayani Kyela mkoani Mbeya.

“Hilo bao lilikuwa la pili katika maisha yangu ya mpira, niliwahi kufunga msimu wa 2018/19 nikiwa Boma wakati tunashinda 1-0 dhidi ya Majimaji kwenye Kombe la Shirikisho, naamini nitaendelea kufunga tena kadri nikipata nafasi itakayoniwezesha kubinuka bila tatizo,” alisema Ngushi.

Advertisement

Kiraka huyo mwenye uwezo wa kucheza namba zote za mbele, aliongeza kutokana na mwanzo mzuri alionao, haoni sababu ya kushindwa kuibuka mfungaji bora iwapo ataendelea kupata nafasi kikosini.

Hata hivyo anabainisha kuwa pamoja na kuwa msimu wa kwanza kwa timu yake kucheza Ligi Kuu, lakini anaiona kwenye nafasi tano za juu mwishoni mwa ligi.

Anakiri pamoja na kazi nzuri anayofanya, lakini vita ya namba kikosini ni nzito kutokana na wapinzani wake wanavyoupiga mwingi na kwamba hawezi kukata tamaa.

“Lolote linawezekana huu ni mpira, kama Mungu akijaalia nikaendelea hivi naweza kuibuka mfungaji bora kwani ndio kitu nakitamani sana ili kuweka rekodi,” alisema Ngushi ambaye anatamani kuzichezea timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam.

Nyota huyo alisema anaamini atafika mbali, kwani ndoto yake ni kuona akicheza soka la kulipwa na la ushindani, huku akieleza kuwa familia yao ni ya watu wanaopenda sana kambumbu.

“Pamoja na kwamba hawachezi soka la ushindani, lakini nyumbani wanapenda mpira, ndoto yangu ni kucheza soka la kulipwa katika timu kubwa,” alisema Ngushi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa timu hiyo, Mohamed Mashango alisema baada ya kuona kipaji cha mchezaji huyo akiwa na Kyela Combine waliamua kumvuta kikosini na kumpa mkataba wa miaka miwili.

Alisema pamoja na mwanzo wake mzuri, iwapo itatokea timu ya kumhitaji, wao hawataweza kumzuia bali watakaa meza moja na kumpa baraka.

“Alicheza Boma miaka ya nyuma, tulimpata akiwa na Kyela Combine ya nyumabani kwao, tunachohitaji ni kuendelea kuibua vipaji, timu itakayomhitaji tutamruhusu kwa utaratibu,” alisema Mashango.

Advertisement