Ngumi ya Carlinhos yawa gumzo nchini

NGUMI ya kiuno aliyoipiga winga wa Yanga, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ dhidi ya beki wa Kengold, Boniface Mwanjonde na kumponza alimwe kadi nyekundu na kutolewa nje kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC) imekuwa gumzo baada ya wadau mbalimbali kuijadili.

Carlinhos alimpiga ngumi beki huyo baada ya kuzidiwa nguvu kwa kupewa ubavu hadi kusukumwa nje ya uwanja, jambo lililoonekana kutomfurahisha staa huyo kutoka Angola ambaye wakati akirejea dimbani akampiga ngumi ya kiuno na kulimwa kadi hiyo. Hata hivyo, Carlinhos aliomba radhi kwa viongozi, makocha, wachezaji wenzake, wanachama na mashabiki wa Yanga.

Tukio hilo, kulingana na kanuni za Ligi Kuu ibara 39 udhibiti wa wachezaji(2.6) Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kupiga /kupigana na mwenzie katika mchezo atasimamishwa michezo mitatu inayofuata ya klabu yake na kulipa faini ya Sh.500,000. ikiwa na maana Carlinhos atakosa mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union na Polisi Tanzania na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Tanzanoa Prisons.

Kitendo hicho, kimewaibua wadau akiwamo nyota wa zamani wa Yanga, Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ akisema alichokifanya Carlinhos ni utoto mno.

Malima alisema alishangazwa pia kuona mchezaji huyo alikuwa anagoma kutoka uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu lakini pia alishangazwa zaidi baada ya kutoka huku akilalamika.

“Nilikuwa uwanjani, timu ipo kwenye presha sana ya ubingwa lakini watu wanabidi wajue kabisa kitendo alichokifanya kitaigharimu timu kutokana na majeruhi waliopo na yeye alikuwa ameshaanza kurejea baada ya kukaa nje kwa muda mrefu,” alisema Malima na kuongeza;

“Carlinhos ni mchezaji mzuri awapo uwanjani akiisaidia timu, anapokosekana ni tabu, viongozi wawe wakali na kukemea vitu kama hivi. Hata hiyo faini alipe mwenyewe ili apate maumivu au kilipiwa basi akatwe katika mshahara.”

Naye Zamoyoni Mogela alisema kitendo alichokifanya Carlinhos kinaigharimu Yanga kipindi hiki washambuliaji wengi majeruhi.